YANGA
kesho inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuivaa Sagrada Esperanca ya
Angola, ikiwakosa wachezaji wake nyota raia wa Zimbabwe, Donald Ngoma na
Thabani Kamusoko kutokana na kuwa na kadi mbili za njano.
Kamusoko
na Ngoma ni msimu wao wa kwanza Yanga wakitokea FC Platinums ya Zimbabwe,
ambapo Ngoma hadi sasa amecheza mechi 45 na kufunga mabao 24 na
Kamusoko amecheza mechi 46 na kufunga mabao tisa katika Ligi Kuu Tanzania
Bara.
Ngoma
mwenye mabao matatu aliyofunga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika alioneshwa
kadi ya pili ya njano katika pambano la marudiano dhidi ya Al Ahly nchini
Misri, ambapo kadi yake ya njano ya kwanza aliipata katika pambano la marudiano
dhidi ya APR Uwanja wa Taifa Dar es Salaam .
Kwa
upande wa Kamusoko mwenye mabao mawili, alioneshwa kadi ya njano katika mchezo
wa marudiano dhidi ya Al Ahly pamoja na pambano la kwanza dhidi ya Cercle de
Joachim.
Hata
hivyo, kukosekana kwa wachezaji hao si pigo sana kwani kocha wa Yanga, Hans
Pluijm ana hazina ya wachezaji ambao amekuwa akiwaanzisha katika mechi
mbalimbali za ligi hiyo hivi karibuni, huku akiwaanzisha benchi Ngoma na
Kamusoko.
Malimi
Busungu ama Paul Nonga mmojawapo anaweza kuchukua nafasi ya Ngoma, huku ile ya
Kamusoko akicheza ama Salum Telela,
Mbuyu Twite, Said Juma Makapu au Haruna Niyonzima.
Yanga
imeangukia katika Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC), baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika
hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2,
ililazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa mabao 2-1 Alexandria,
Misri.
Yanga
ilizitoa Cercle de Joachim ya Mauritius kwa mabao 3-0, ikishinda 1-0 ugenini na
2-0 nyumbani kabla ya kuitoa APR ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda
2-1 Kigali na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
Kwa
upande wao, Sagrada Esperanca katika Raundi ya Awali waliitoa Ajax Cape Town ya
Afrika Kusini kwa mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0
nyumbani.
Katika
Raundi ya kwanza waliitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa mabao 2-1, ikishinda 1-0
nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini na kwenda hatua ya 16 Bora, ambako
waliitoa V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 wakishinda 2-1 ugenini
na 2-0 nyumbani.
Vingilio
katika mchezo huo utakaochezeshwa na
waamuzi kutoka Ghana, cha juu ni Sh
30,000 na chini ni Sh 5,000.
Akitangaza
vingilio hivyo, Ofisa Uhusiano wa Yanga, Jerry Muro alisema vingilio vingine ni
Sh 20,000 na Sh 7,000.
Pia
alisema kukosekana kwa Ngoma na Kamusoko si tatizo na kwamba kocha ameshafanyia
kazi suala hilo na mashabiki wasiwe na hofu, Yanga ina wachezaji wengi wenye
uwezo mkubwa.
Kwa
upande wake, Pluijm alisema amewapanga vyema vijana wake na kuwaomba mashabiki
kujitokeza kwa wingi kuwaunga mkono katika mchezo huo.
“Tupo
vizuri, tumejipanga kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wetu,” alisema Pluijm.
No comments:
Post a Comment