Pages

Saturday, October 31, 2015

TASWA YAMPONGEZA MAGUFULI

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), kinatoa pongezi za dhati kwa Dk. John Magufuliwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano ya Tanzania.
 
TASWA imepokea kwa furaha ushindi huo wa Dk. Magufuli, ikiamini atawapa furaha wanamichezo katika masuala mbalimbali kama alivyofanya mtangulizi wake Rais, Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake wa kuwatumikia Watanzania kwa mujibu wa katiba na ataanzia pale mtangulizi wake alipoishia kuhusiana na michezo kwa ujumla.
 
Kutokana na hali hiyo tunampongeza Rais Mteule Dk. Magufuli na Makamu wake, Samia Suluhu Hassan, ambaye atakuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa wa Makamu wa Rais hapa nchini.
 
Tunaamini watakuwa tumaini kubwa la wanamichezo na tunaahidi kuwapa ushirikiano wa kutosha ili watekeleze majukumu yao ipasavyo upande wa michezo.
 
Pia TASWA inawapongeza wadau wote wa michezo waliochaguliwa kwa nafasi mbalimbali za Ubunge na Udiwani na tunaamini ushindi wao utakuwa mwanzo mzuri katika kusaidia michezo hapa nchini.
 
Tunawapongeza pia wale ambao si wanamichezo, lakini walitumia mgongo wa michezo na wanamichezo kutafuta uongozi wa kisiasa katika nafasi za Ubunge na Udiwani, wakiahidi watasaidia michezo. Nao tunawapongeza na tunasubiri utekelezaji wa ahadi zao.
 
Wanasiasa ndiyo wanaounda Serikali, tena wao ndio wanaofanya uamuzi kutokana na nafasi zao. Watendaji ni wataalamu, na kazi yao ni kushauri au kutoa ushauri. Ushauri ni kitu kimoja, na ushauri kufanyiwa kazi ni kitu kingine pia.
 
Hivyo basi tunaamini wanasiasa walioingia wakitokea kwenye michezo wanajua matatizo yaliyoko huko kwa kiasi kikubwa kuliko mwingine yeyote, hivyo wanaweza kusaidia kwa kiasi fulani mawazo ili michezo ipige hatua.
 
Ahsanteni,
 
Juma Pinto
Mwenyekiti TASWA
30/10/2015

No comments:

Post a Comment