Pages

Thursday, October 22, 2015

JACKSON MAYANJA KOCHA WA KWANZA KUTIMULIWA MSIMU HUU 2015-2016

KIKAO cha Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Coastal Union kilichoketi juzi kwa saa tatu kilitoka na mapendekezo wa kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo,Jackson Mayanja kutokana na kutokuwepo kwa mwenendo wa matokeo mazuri kwa timu hiyo tokea alipokabidhiwa.
Kocha Mayanja alikabidhiwa kikosi hicho cha Wagosi wa Kaya baada ya kumalizika msimu wa ligi kuu uliopita akichukua mikoba ya Jamhuri Kihwelu “Julio” ambaye aliinusuru timu hiyo na kushuka daraja ikimaliza ikiwa nafasi tano za juu kwenye msimamo.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kikao hicho,Ofisa Habari wa Coastal Union,Oscar Assenga alisema kuwa kikao hicho kilikutana chini ya Mwenyekiti wao Dr.Ahmed Twaha ambapo pamoja na mambo mengine kilikuwa na agenda kadhaa lakini kubwa ikiwa sababu za timu hiyo kutokufanya vizuri kwenye michuano ya Ligi kuu.
Assenga alisema kuwa agenda hiyo ilikuwa mzito kwa wajumbe kutokana na timu usajili makini uliofanywa kwa wachezaji lakini wakaonekana kushindwa kuendana na kasi iliyokuwa ikitakiwa ili kuweza kuipa mafanikio timu hiyo kwenye mechi zao.
Alisema kuwa sababu kubwa zilizopelekea kuachana na kocha huyo zinatokana na aina ya ufundishaji wake kutokuendana na kasi ya timu hiyo kutokana na wachezaji kukosa stamina hali iliyopelekea kushindwa kucheza kwa mafanikio kwenye mechi zao.
“Lakini hata ukiangalia wakati wa mazoezi wachezaji wetu wamekuwa wakichezeshwa nusu uwanja huku kwenye mechi za ligi kuu wanatakiwa kucheza uwanja mzima pamoja na timu yetu kupoteza stamina na wachezaji kupoteza umakini kutokana na aina ya ufundishaji wake,”Alisema
Aidha alisema kuwa baada ya mechi ya leo(jana) timu hiyo itakuwa chini ya Mbwana Bushiri Akisaidiana na Kamati ya Ufundi ya timu hiyo ambao watakuwa na jukumu la kuiandaa timu hiyo kuelekea mapambano ya Ligi kuu soka kwenye mechi zinazofuata.

Hata hivyo alisema kuwa tayari Mwenyekiti wa timu hiyo,amemuagiza Katibu Mkuu wa timu hiyo,Kassim El Siagi kuwaandikia barua Kamati ya Ufundi haraka iwezekanavyo ili waweze kutambua majukumu yao hayo mpaka atakapopatikana Kocha Mpya.
mwisho
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO YA COASTAL UNION.

No comments:

Post a Comment