Pages

Friday, September 4, 2015

STARS YAAPA KUFA NA NIGERIA KESHO


TIMU ya soka ya taifa, Taifa Stars kesho itacheza na Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.

Kocha Mkuu wa Stars, Charles Mkwasa amesema  kuwa Nigeria inafungika endapo wachezaji wake watatimiza majukumu yao kama alivyowafundisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Mkwasa alisema anawashukuru watanzania kumuonesha ushirikiano na kuwaomba kujitokeza kwa wingi leo.

“Nawashukuru Watanzania kwa ushirikiano wanaouonesha tangu tukiwa kambini Uturuki hadi sasa tumerejea nyumbani tunaona jinsi  wako pamoja na timu yao,” alisema Mkwasa.

Pia alisema mechi itakuwa nzuri, ikiwa kila mtu atatekeleza majukumu yake, wanaweza kuibuka na ushindi kwa sababu hakuna timu isiyofungika ila inategemea na wao wamejipangaje kuweza kushinda mchezo huo.

“Hakuna timu ndogo wala kubwa siku hizi, timu yoyote unayokutana nayo unatakiwa kupambana hadi mwisho kuhakikisha unashinda, kama wao wanatuona sisi ni timu ndogo sawa lakini sisi pia hatuogopi, tunajua Nigeria ni timu kubwa ila tunawaheshimu kutokana na ubora walionao,” alisema Mkwasa.

Mkwasa alibainisha mchezo utakuwa mgumu ila kwa vile wamejiandaa tangu kambi ya Uturuki  watapambana mpaka mwisho kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwa hali na mali ili kuwapa faraja watanzania.

Kukosekana kwa golikipa namba moja wa Nigeria, Vincent Enyeama, Mkwasa alisema watatumia nafasi hiyo kuhakikisha wanafanya mashambulizi lakini akasisitiza kuwa wao wamejipanga kuikabili Nigeria kama timu na siyo mchezaji mmoja mmoja.

 “Tutawakabili Nigeria kama timu na si mchezaji mmoja mmoja, lakini kutokuwepo kwa kipa wao namba moja inaweza kuwa ni faida kwetu japokuwa hata golikipa atakayedaka anaweza kuwa na kiwango cha juu kumpita Enyeama lakini hapati nafasi kwenye timu,” alifafanua Mkwasa.

 Mkwasa alisema safu ya ushambuliaji wamefanya mazoezi ya kutosha juu ya kufunga wakiwa Uturuki na hata kwenye mazoezi baada ya kurejea Tanzania, ana imani washambuliaji wake watafanya kile alichokielekeza kwani timu ilicheza mechi tano bila kufunga hata bao moja lakini tangu ameanza kuifundisha imefunga mabao mawili kwenye mechi mbili japo haikupata ushindi.

 Kwa upande wa kocha Sunday Oliseh, huu utakuwa mtihani wake wa kwanza baada ya kurithi mikoba ya kocha Stephen Keshi aliyeachia ngazi Julai.

 Ingawa Stars iko nyuma ya Nigeria kwa nafasi 87 katika viwango vya ubora vya FIFA, bila shaka  itatoa changamoto kubwa dhidi ya mabingwa hao wa zamani wa Afrika ambao wameanza kuunda upya timu yao kupitia Oliseh.

Oliseh atakuwa akiangalia pia mchezo wa kundi ‘G’ kati ya Misri na Chad ambapo Misri wanaongoza kundi kwa tofauti ya mabao.

Mchezo huo utaanza saa 10:30 na  utachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda ambao ni Louis Hakizimana  (kati), Honore Simba (mwamuzi msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (mwamuzi msaidizi), Abdoul Karim Twagiramukiza (mwamuzi wa akiba) na kamishna ni Charles Masembe kutoka nchini Uganda.

Viingilio vya mchezo ni VIP A Sh 40,000, VIP B Sh 30,000, VIP C Sh15,000, Rangi ya Machungwa (Orange) Sh 10,000, na viti vya rangi ya Bluu na Kijani Sh 7,000.

No comments:

Post a Comment