Pages

Tuesday, September 22, 2015

MBASHA AACHIWA HURU NA MAHAKAMA, BAADA YA WALALAMIKA KUSHINDWA KUDHIBITISHA MASHITAKA YA UBAKAJI







HATIMAYE Mume wa muimbaji wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, Emmanuel Mbasha (32) ameachiwa huru jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, baada ya upande wa mshitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka ya kubaka yaliyokuwa yanamkabili.

Baada ya kuachiwa huru, Mbasha alitoka mahakamani hapo ambapo alipiga magoti  na kulia huku amenyanyua mikono juu ishara ya kumshukuru Mungu.

Akisoma hukumu hiyo jana kuanzia  saa 4:45 hadi saa 5:15 asubuhi asubuhi, Hakimu Mujaya alisema Mbasha alikabiliwa na mashitaka mawili ya kubaka.

Alisema kwamba mahakama hiyo ilisikiliza mashahidi sita wa upande wa mashitaka akiwemo muhangwa wa tukio hilo ambaye ni shemeji wa Mbasha mwenye umri wa miaka 17 na Flora.

Hukumu hiyo ambayo ilisikilizwa katika chumba cha siri (chamber Court) Hakimu Mjaya alisema shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, ambaye ni shemeji wa mbasha aliiambia mahakama kuwa Mei 23 mwaka jana alibakwa na Mbasha nyumbani kwake, Tabata Kimanga baada ya Flora kwenda kuchukua CD za nyimbo zake.

Pia alisema shahidi huyo alidai alibakwa kwa mara ya pili katika gari aina ya Ipsum walipokuwa wanatoka kumtafuta Flora ambaye alikuwa haonekani nyumbani.

Akipitia ushahidi wa Daktari wa Hospitali ya Amana, Migole Mtuka, hakimu huyo alisema, daktari huyo alidai ndiye alimfanyia vipimo msichana huyo na kuwa hakuona dalili zozote za kuingiliwa kimwili na Mbasha.

Alisema daktari huyo alidai kuwa binti huyo alifika hospitalini hapo Mei 26, mwaka jana, kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na baada ya kumtaka kwenda maabara, hakwenda bali alitoroka  na kurejea Juni 3, mwaka jana, baada siku nane kupita.

Hata hivyo, Hakimu Mjaya alisema kupitia mashahidi wote mahakama iliona mapungufu katika ushahidi huo ambapo ilimuona mshitakiwa hana hatia.

‘’Kupitia ushahidi huu mahakama imebaki na maswali kama kweli umebaka au la. Kwa hivyo upande wa mashitaka umeshindwa kuthibitisha mashitaka haya bila ya kuacha shaka na mahakama inakuachia huru,’’ alisema Hakimu Mjaya.

Mbasha  alifika mahakamani hapo akiongozana na mdogo wake wa kiume pamoja na Wakili wake, Mathew Kakamba.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama hiyo, Mbasha alisema Mungu ni mwema huku akifuta machozi na kuwaambia waandishi kuwa watawasiliana.

Awali, Mbasha alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo Juni 17 mwaka jana akitokea Kituo cha Polisi Tabata, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Wilberforce Luhwago.

Jalada la kesi hiyo liliamishwa kwa Hakimu Mkazi, Flora Mujaya baada ya Hakimu Luhwago kuwa na majukumu mengine ya kazi.

Katika kesi hiyo, Mbasha alikabiliwa na mashitaka mawili ya ubakaji ambapo ilidaiwa alitenda makosa hayo maeneo ya Tabata Kimanga, jijini Dar es Salaam.
Katika mashitaka ya kwanza ilidaiwa  Mei 23, mwaka jana  maeneo hayo, Wilaya ya Ilala, kinyume cha sheria za nchi,  alimbaka msichana huyo.
Pia ilidaiwa kuwa Mei 25, mwaka jan, maeneo la Tabata Kimanga nyumbani kwa mshitakiwa  alimbaka tena mlalamikaji huyo.
Hata hivyo, mshitakiwa alikana mashitaka hayo na kuwa nje kwa dhamana  baada ya kulala siku moja katika mahabusu ya Keko.
Mwishooo

No comments:

Post a Comment