Pages

Tuesday, September 8, 2015

KAGERA SUGAR KUTUMIA UWANJA WA ALI HASSAN MWINYI TABORA NA MKUTANO MKUU TFF DISEMBA



WAKATI pazia la Ligi Kuu Tanzania bara msimu wa 2015/2016 likitarajiwa kufunguliwa jumamosi, klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera itatumia  Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kwa mechi zake za nyumbani badala ya Uwanja wa Kaitaba, Kagera.
Akizungumza na wandishi wa habari, Afisa habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Baraka Kizuguto alisema mabadiliko hayo yamefanyika kupisha shughuli ya uwekaji nyasi bandia inayoendelea kwenye uwanja wao wa Kaitaba mjini Bukoba unaofanywa na wataalamu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).
“Kagera Sugar watatumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kwenye mechi zake za nyumbani ambazo ni dhidi ya Toto Africans utakaochezwa Septemba 26, JKT Ruvu Septemba 30, Tanzania Prisons Octoba 4 na Yanga Octoba 31”, alisema Kizuguto.
Mechi zingine zitaendelea kawaida ambapo jumamosi Septemba 12, 2015 kutakuwa na michezo saba itakayochezwa katika viwanja tofauti nchini.
Ndanda FC ya Mtwara watakua wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nag’wanda Sijaona mjini Mtwara, Wana kimanumanu African Sports watawakaribisha Simba katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Wana Lizombe Majimaji wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Azam FC watakua wenyeji wa Tanzania Prisons katika uwanja wa Chamazi Complex, Stand United FC chama la wana watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Ligi Kuu itaendelea jumapili kwa mchezo mmoja utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mabingwa watetezi Yanga watawakaribisha wagosi wa kaya Coastal Union.
Wakati huo huo kikao cha Kamati ya Utendaji cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichokaa Septemba 06, 2015 Mkutano Mkuu wa TFF kufanyika  Disemba 19-20, 2015.
Ajenda za Mkutano huo zitakuwa ni kwa mujibu wa katiba ya TFF.

No comments:

Post a Comment