Pages

Friday, August 7, 2015

MASHABIKI WAMBAKISHA COUTINHO YANGA


Andrey Coutinho na Geofrey Mwashiuya


MASHABIKI wa Yanga wamemwokoa  kiungo Mbrazil Andrey Coutinho asitemwe Yanga baada ya kumpigia simu Manji na kumtaka mchezaji huyo aendelee kuwepo kwenye kikosi chao.
Awali baada ya Yanga kuondolewa kwenye mashindano ya Kagame, Countinho  alikuwa aondoke pamoja na beki Mghana, Joseph Tetteh Zuttah lakini mashabiki walimpigia simu Rais wa Yanga, Yusuph Manji, wakimtaka mchezaji huyo asiondoke kwenye kikosi kwani kiwango chake kipo juu.
Akizungumza bila kutaka jina lake kuandikwa gazetini, chanzo hicho kilisema baada ya mashabiki kusoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa Coutinho anaondoka waliamua kumpigia simu Manji na yeye kuwasiliana na Katibu Mkuu, Dr. Jonas Tiboroha akimwambia ahahakishe usajili unafanyika vizuri pia mchezaji huyo asiondoke.
“Mashabiki walimpigia simu Manji na yeye akamwagiza Tiboroha awasiliane na benchi la ufundi kuhakikisha usajili unafanyika vema lakini kiungo Countinho abaki kuendelea kuichezea Yanga”, kilisema chanzo hicho.
Baada ya Yanga kutolewa katika robo fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame ilikitathmini kikosi chake na kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
 Coutinho alijiunga na Yanga msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
Mbrazil huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
Tayari Yanga wamewasajili kiungo Thabani Kamusoko ambaye alikuwa nahodha wa FC Platinum ya Zimbabwe kuziba nafasi ya Mliberia, Kpah Sherman aliyeuzwa nchini Afrika Kusini kwenye klabu ya Mpumalanga inayoshiriki ligi kuu ya nchini humo na beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou ambaye amechukua nafasi ya beki Zuttah.
Wachezaji wa kigeni Yanga ni Mkongo, Mbuyu Twite, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.

No comments:

Post a Comment