Pages

Tuesday, June 2, 2015

U13 KUTIMUA VUMBI MWANZA JUNI 7


Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Julai 7 mwaka huu litafungua mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 13 jijini Mwanza kwa mikoa yote ya Tanzania kwa lengo la kung’amua vipaji kwa ajili ya kuunda timu ya Taifa  ya vijana wenye umri huo.

Mashindano hayo yatakayofanyika kwa kipindi cha wiki moja, yatafanyika katika viwanja vya CCM Kirumba na Alliance vyote vilivyopo jijini Mwanza, na maandalizi ya michuano hiyo yamekamilika na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa mkoa Mwanza.

Jopo la makocha litakua katika viwanja hivyo kusaka vipaji kwa lengo la kuanza kuiandaa timu ya Taifa ya vijana wenye umri wa miaka 13, ili ifikapo mwaka 2019 waweze kuiwakilisha Tanzania katika fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 zitakazofanyika hapa nchini.

Mapema wiki iliyopita Shirikisho la Soka barani Afrika - CAF liliipa Tanzania uenyeji wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 zitakazofanyika mwaka 2019.

TFF katika kuhakikisha inafanya vizuri katika soka la vijana, mapema mwezi Aprili iliendesha kozi ya waamuzi vijana jijiji Dar es salaam, ambapo vijana 36 walishiriki kozi hiyo na kutunukiwa vyeti.

Aidha TFF ina programu ya vijana chini ya miaka 15 ambayo ilianza kambi mwezi Aprili mwaka huu, na inatarajiwa kucheza michezo ya kirafiki katika mikoa saba nchini kati ya mwezi Juni na Agosti, kabla ya mwezi Disemba kusafiri katika nchi Malawi, Zambia, Zimbabwe, Bostwana na Afrika Kusini.

Kikosi hicho cha umri chini ya miaka 15 kinajiandaa na kuwania kufuzu kwa fainali za Vijana Afrika mwaka 2017 ambapo katika ziara hizo za mikoani, walimu watatumia nafasi hiyo kungamua na kuongeza vijana wengine katika 
kikosi.

No comments:

Post a Comment