Pages

Saturday, June 20, 2015

SIMBA NA YANGA RUKSA KUSAJILI SABA WA KIGENI LAKINI LAZIMA TFF ILIPIWE ADA YA DOLA 2000 KILA MMOJA



KAMATI ya Utendajia ya Shirikisho la soka Tanzania (TFF) imepitisha ombi la usajili wa wachezaji saba wa kigeni kwa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.
Hicho kilikuwa kilio kikubwa kwa klabu za ligi, hasa Yanga, Azam na Simba ambazo ndizo zinazosajili wachezaji wengi wa kigeni.
Kabla ya TFF kupitisha uamuzi huo, klabu ziliruhusiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni bila kulipa TFF ada lakini sasa watalazimika kulipia kila mchezaji wa kigeni atakayesajiliwa.
Habari kutoka ndani ya kikao cha kamati ya utendaji kilichofanyika mjini Zanzibar leo, zilisema mvutano ulikuwa mkali wa ama kusajili wachezaji watano ama saba.
“Mjadala ulichukua muda mrefu sana, lakini kama unavyojua hiki kitu klabu kubwa zinamaslahi nacho, na ndio waliotoa ushawishi kwa wajumbe wengi kutaka usajili wa wachezaji saba mwisho tukakubaliana hivyo na hao saba wanaruhusiwa kucheza wote kwenye mechi moja,” alisema mtoa habari wetu kutoka ndaniya kikao hicho.
 Lakini timu zimewekewa sharti gumu ambalo  ni lazima kila mchezaji alipiwe ada ya dola za Marekani 2000 kwa mwaka lakini pia mchezaji anayesajiliwa kutoka nje lazima awe anacheza timu ya taifa  ya nchi husika au Ligi Kuu.
Hii si mara ya kwanza kwa klabu za Ligi Kuu kuruhusiwa kusajili wachezaji zaidi ya watano, miaka ya nyuma ilikuwa ikisajili wachezaji kumi na kuruhusiwa kutumia watano kwenye mechi moja, lakini hakukuwa na masharti yoyote ya aina ya wachezaji wa kusajiliwa, hali iliyofanya klabu kusajili wachezaji wasio na uwezo, ama majeruhi ambao wakifika nchini hushindwa kutoa msaada kwa klabu husika.
Mwaka 2007 kulifanyika kangamano Bagamayo ambapo baadhi ya maazimio kwenye kongamano lile ni kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni ambapo ilikubalika mpaka msimu uliopita klabu zisajili wageni watano na watakaotumika kwa mechi moja wawe watatu.
Lakini hali imekuwa tofauti baada ya baadhi ya klabu kudai kuongezewa idadi ya usajili wa wachezaji wa kigeni ili zifanye vizuri kwenye michuano ya kimataifa.

No comments:

Post a Comment