Pages

Saturday, June 20, 2015

JKT BINGWA WA JUMLA MASHINDANO YA MAJESHI


Mkurugenzi wa Mafunzo na Ufundi, Makao Makuu ya Jeshi, Brigedia Jenerali, Blaus Masanja akimkabidhi kombe naodha wa JKT, Said Madega baada ya kuibuka mabingwa kwa kuifunga Ngome bao 1-0


TIMU ya  kombaini ya soka ya JKT imetwaa kombe la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,  (CDF) kwenye fainali zilizofanyika kwenye Uwanja wa Twalipo  uliopo kambi TAU, Kurasini,  jijini Dar es Salaam jana.
Kombaini ya JKT inayofundishwa na kocha koplo Bryson Haule  ilicheza na timu ya Ngome inafundishwa na kocha Mteule daraja la kwanza,  Steven Matata na kufanikiwa kuifunga Ngome bao 1-0 lililofungwa na Idd Mbanga dakika ya 45 kwa kichwa.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko lakini mabadiliko hayo hayakuweza kubadilisha matokeo kwani hadi dakika ya 90 JKT walitawazwa mabingwa wa kombe la Mkuu wa majeshi ya Ulinzi 2015.
Akizungumza wakati wa kufungua mashindano hayo, Mkurugenzi wa Mafunzo na Ufundi, Makao Makuu ya Jeshi, Brigedia Jenerali, Blaus Masanja alisema kuwa nia ya jeshi ni kuinua na kuendeleza michezo ili kukuza michezo kama ilivyokuwa awali.
“Jeshi tumejipanga kurudisha hadhi ya michezo kwa majeshi yetu kama ilivyokuwa mwanzo kwa kutumia kambi na vikosi mbalimbali vya jeshi”, alisema Brigedia Jenerali Masanja ambaye alimwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Generali Davis Adolf Mwamunyange.
Mashindano hayo ambayo ni mara ya pili kufanyika tangu yaanzishe yalikuwa maalum kwa ajili ya kuchangua timu itakayowakilisha nchi kwenye mashindano ya majeshi kwa nchi za Afrika Mashariki yatakayofanyika Agosti nchini Uganda.
Mashindano haya yalishirikisha michezo ya riadha, netiboli, wavu, mpira wa mikono, kikapu na mbio za nyika kwa jinsia zote.
Mshindi wa pili kwa soka ilichukuliwa na Ngome huku nafasi ya tatu AFC wakati bingwa kwa upande wa mpira wa mikono ni JKT, mshindi wa pili ni Ngome na mshindi wa tatu ilichukuliwa na Nyuki.
Mchezo wa kikapu kwa wanaume bingwa ni JKT, nafasi ya pili ilichukuliwa na Ngome, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na  302 KV wakati bingwa kwa mchezo wa netiboli wanawake ni JKT, mshindi wa pili ni Ngome.

No comments:

Post a Comment