Pages

Tuesday, May 26, 2015

KASEKE AMWAGA WINO YANGA, AKABIDHIWA JEZI


UONGOZI wa Yanga umemtambulisha rasmi mchezaji wake mpya Deus Kaseke na kumkabidhi rasmi jezi namba nne iliyokuwa ikivaliwa na Rajab Zahir ambaye mkataba wake umekwisha. Kaseke alisajiliwa juzi kwa mkataba wa miaka miwili, akitokea Mbeya City alikotumika kwa miaka minne na mkataba wake umemalizika mwishoni mwa msimu huu.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro, Zahir mkataba wake umekwisha hivyo wanaendelea na mazungumzo naye na wakati wowote wataweka wazi kama watamsajili au aende zake. Muro alisema Kaseke alikuwa ni bora ndio maana walivutiwa na kipaji chake wakiamini anaweza kuisaidia timu kufanya vizuri msimu ujao.
“Ni furaha kubwa kuwa na mchezaji mwenye kipaji kikubwa tunaamini atatusaidia Yanga kufanya vizuri, ni mchezaji mzuri amekuja kucheza katika timu ya kimataifa na atakuwa wa kimataifa,” alisema.
Alisema mchezaji huyo ni mzalendo na ameonesha uwezo mkubwa msimu uliopita ndio maana wamevutiwa naye.
Kwa upande wake, Kaseke alisema amefuhi kupata nafasi ya kuitumikia klabu hiyo na kuahidi kuendelea kuonesha juhudi pale alipoachia na kuiwezesha Yanga kufanya vizuri.
“Nawashukuru Mbeya City hadi mkataba wangu ulipoisha tulifanya kazi vizuri, lakini pia nafurahia sehemu nilipo sasa kwani ndoto yangu imetimia nilitamani kucheza michezo ya kimataifa,”alisema.
Kaseke ambaye amezaliwa miaka 21 iliyopita, ana uwezo wa kucheza namba saba, 11 na 10 na amesajiliwa na timu hiyo ili kuziba nafasi iliyoachwa na Mrisho Ngassa aliyesajiliwa na Free State Stars.
Alisema atapambana kwa uwezo wake kuonesha juhudi ili kupata namba kwenye kikosi cha kwanza na kufanya vizuri zaidi katika michezo ya kimataifa.
Muro alisema wachezaji wengine wataendelea kusajiliwa siku za karibuni na kutambulishwa, hivyo kuondoa uvumi kuwa wamemsajili mchezaji fulani.
Miongoni mwa wachezaji wanaopewa nafasi ya kusajiliwa na Yanga ni Haruna Chanongo, ambaye mkataba wake umemalizika Simba.
Pia, alitangaza rasmi kuwasajili kwa mara nyingine kiungo mchezeshaji Haruna Niyonzima kwa mkataba wa miaka miwili, Mbuyu Twite mwaka mmoja na Deogratias Munishi miaka miwili.

No comments:

Post a Comment