Chama cha
kandanda mkoa wa Dar es salaam DRFA,kimeeleza kusikitishwa kwake na kifo cha
mchezaji kiungo wa zamani wa klabu ya simba na timu ya taifa-Taifa
Stars,Christopher Alex maarufu kama Masawe,kilichotokea
leo (februari 22 mwaka huu),katika Hospitali ya Mirembe Dodoma.
Mwenyekiti wa
DRFA,Almas Kasongo,amemuelezea marehemu Christopher kuwa ni mchezaji aliyevuma
enzi za uhai wake na kuiletea heshima kubwa klabu yake ya Simba na Taifa Kwa
ujumla,pale walipofanikiwa kuisukumiza nje ya michuano ya afrika klabu ya Zamalek
na kuivua ubingwa miamba hiyo ya soka ya kaskazini mwaka 2003.
Kiungo huyo
aliyeanza kuvuma katika miaka ya 2000,amefariki dunia kutokana na kusumbuliwa
kwa muda mrefu na ugonjwa wa kifua kikuu (TB).
Marehemu Christopher
Alex, alizaliwa Septemba 12 mwaka 1975,na kupata elimu yake ya msingi katika
shule ya msingi Uhuru na kumaliza katika shule ya Chamwino huko Dodoma mwaka
1993,na alianza kucheza mpira kwenye timu ya Daraja la nne Chamwino UTD na
baadaye daraja la tatu akiwa na kikosi cha Aston Villa nayo ya Dodoma.
Mwaka 1999-2001
ameitumikia klabu ya CDA ya Dodoma,kabla ya kutimkia klabu ya Reli mwaka 2002
na baadaye kujiunga na wekundu wa msimbazi Simba,Marehemu ameacha mtoto mmoja aitwaye
Alex.
Kasongo,kwa
niaba ya kamati ya utendaji ya DRFA,wametoa ubani wa shilingi laki mbili
(200,000/=) kwa familia ya marehemu,na kuwataka mashabiki wa soka na watanzania
kwa ujumla kuungana pamoja katika kuifariji familia hiyo kwenye kipindi hiki
kigumu cha majonzi.
No comments:
Post a Comment