Pages

Saturday, December 13, 2014

SIMUYU YAANZA VIBAYA COPA COCA COLA

Waziri wa habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dr Fenela Mukangara akipiga mkwaju wa penati kuashiria  uzinduzi rasmi wa mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 15 ya Copa Coca-Cola ngazi ya Taifa, jijini  Dar-es-salaam leo

TIMU ya soka ya mkoa wa Simiyu imeanza vibaya mashindano ya Copa-Coca-Cola ngazi ya taifa baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa vijana wa Mkoa wa Kigoma kwenye mchezo wa ufunguzi uliochezwa katika uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam jana.
Kigoma walipata bao la kwanza mapema kwenye dakika ya nane kupitia kwa Juma Swalehe, huku Juma Zuberi akiongeza bao la pili dakika ya 30 na Idrisa Akilimali alihitimisha karamu ya mabao kwa Kigoma kwa kufunga bao safi mnamo dakika ya 57, bao la kufutia machozi la Simiyu lilifungwa na Kaluona Abdallah katika dakika ya 88 ya mchezo huo.
Michuano hiyo ilizinduliwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Fenella Mukangara ambaye aliwashauri makocha wa timu kutumia michuano ya Copa-Coca-Cola kama changamoto ya kuibua vipaji vipya katika timu zao kwa wasichana na wavulana.
Mukangara aliwaasa vijana kuhakikisha wanajituma kulitangaza taifa la Tanzania katika michuano mabalimabli ya  kimataifa. “Nina furaha sana kuona wasichana pia wakijumuishwa katika michuano hii ya Copa-Coca-Cola na pia natoa shukrani zangu za dhati kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa kuhakikisha kuwa soka la wanawake linakuwa hapa nchini”, Mukangara alisema.
Mukangara pia aliwasisitiza washiriki wote wa michuano hiyo kuhakikisha kuwa wanazingatia nidhamu ya mchezo uwanjani. “Tuna imani kuwa washiriki wote mtazingatia sheria za mchezo huu kama inavyagizwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA)”, Aliongeza Mukangara.
Naye Meneja wa Coca-Cola nchini  Yebeltal Getachew alielezea nia yao ya dhati katika kuendeleza michuano hiyo ya Copa-Coa-Cola nchini. Wachezaji wanaofanya vizuri katika michuano hii hupelekwa nchini Afrika Kusini kwa mafunzo zaidi.
Copa-Coca-Cola ni michuano pekee ambayo huanzia ngazi ya chini kabisa na baadaye ngazi ya Taifa ikishirikisha mikoa yote ya Tanzania bara pamoja na Zanzibar.
Kwa upande wake Rais wa TFF Jamal Malinzi aliwaonya viongozi wa timu zote zinazodanganya umri na kusisitiza kuwachukulia hatua za kinidhamu. “Katika kuonesha umakini katika michuano hii tumewaondoa wachezaji 87 kutoka katika mikoa ya Mbeya na Lindi kutokana na kudanganya umri”, Malinzi alisisitiza.


Michuano ya Copa-Coca-Cola itafikia tamati mnamo Desemba 20, mwaka huu, katika Uwanja wa kumbukumbu ya Karume jijini Dar es salaam.

No comments:

Post a Comment