Pages

Thursday, December 18, 2014

KOCHA VAN GAAL, VAN PERSIE WAZOA TUZO ZA JUU KWAO UHOLANZI

 Louis van Gaal amesimikwa kama ndie Kocha Bora wa Mwaka huko kwao Holland baada ya kuiongoza vyema Nchi yake kufika Nusu Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil Mwezi Julai. Van Gaal, ambae aling’atuka kama Kocha wa Holland mara baada ya Kombe la Dunia na kutua Manchester United kama Meneja mpya, alipewa Tuzo yake hiyo ya juu hapo Jana huko Mjini Amsterdam wakati wa Hafla maalum ya Wanamichezo. Van Gaal ndie aliekuwa kiini cha kuiongoza Holland kufika Nusu Fainali za Kombe la Dunia huko Brazil ambapo walitolewa kwa Mikwaju ya Penati na Argentina lakini wakafanikiwa kutwaa Nafasi ya 3 kwenye Kombe la Dunia baada ya kuichapa Brazil 3-0. Kocha huyo mwenye Miaka 63 ambae pia aliwahi kuiongoza Holland kati ya Mwaka 2000 na 2002 alihamia Man United Mwezi Julai na kumwachia wadhifa wa kuiongoza Holland Guus Hiddink. Sambamba na Van Gaal kutwaa Tuzo, Mchezaji wake wa Man United na ambae pia ni Nahodha wa Holland, Robin van Persie, nae pia alitunukiwa Tuzo kwenye Hafla ya hiyo Jana. Van Persie alipewa Tuzo ya Mchezo Bora wa Mwaka kutokana na Bao lake safi alilofunga kwa Kichwa wakati Holland inawatwanga waliokuwa Mabingwa wa Dunia Spain Bao 5-1 katika Mechi ya ufunguzi ya Kundi lao kwenye Kombe la Dunia huko Brazil Mwezi Juni.

Bao hilo pia lipo kwenye kinyang’anyiro cha kuwania Tuzo ya FIFA ya kuwania Bao Bora la Mwaka Duniani ambapo Mshindi wake kati ya Wagombea Watatu atatangazwa Januari 12.

No comments:

Post a Comment