Pages

Wednesday, December 31, 2014

KLABU YA SIMBA YAMTIMUA KOCHA PATRICK PHIRI

KLABU ya Simba imeamua kumfungashia virago Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Phiri kutoka Zambia.
Habari kutoka ndani ya Simba zimeeleza jana kuwa, kocha huyo alitarajiwa kukabidhiwa rasmi barua ya kuvunja mkataba wake jana.
Kwa mujibu wa habari hizo, Simba imeamua kuvunja mkataba na Simba kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Simba imemfungashia virago Phiri siku chache baada ya timu hiyo kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Awali, kocha huyo aliingoza Simba kuichapa Yanga mabao 2-0 katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyochezwa kwenye uwanja huo.

Phiri alikaririwa jana kwenye mitandao ya kijamii akithibitisha kutaarifiwa kuhusu kuvunjwa kwa mkataba wake.
Kocha huyo amesema ni suala la kawaida kumtokea kocha, hivyo hana kinyongo na uongozi wa klabu hiyo.
"Wamenitaarifu kuhusiana na kuachishwa kazi, hili si jambo jipya, ingawa niliona tungeweza kubadilisha mambo.
"Najua Simba wanataka kufanya vizuri, hivyo siwezi kumlaumu mtu na utaona mwendo wa timu yetu ulivyokuwa," alisema Phiri.
Phiri amesema anatarajia kurejea kwao baada ya kulipwa madai yake na uongozi wa Simba. Hakutaja kiasi anachoidai klabu hiyo kama mishahara na fidia ya kuvunjwa kwa mkataba.

No comments:

Post a Comment