Pages

Saturday, February 8, 2014

YANGA YAFANYA KWELI TAIFA, YAWASHINDILIA WACOMORO 7-0




WACOMORO ni wateja wazuri kwa Yanga na hawana ujanja wa kufurukuta kwa namna yoyote mbele ya timu hiyo ya  Dar es Salaam.

Hivyo ndivyo unavyoweza kuzungumzia matokeo ya mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga na Komorozine ya Comoro uliofanyika leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 7-0.

Yanga iliyoenda mapumziko ikiwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa dakika ya 13 na Nadir Haroub dakika ya 20 ilitawala sehemu kubwa ya mchezo huo, huku wapinzani wao wakionekana wachovu.

Ngassa alifunga bao hilo kwa kichwa akiunganisha krosi ya Mbuyu Twite, huku bao la Haroub pia likifungwa kwa kichwa kutokana na krosi ya David Luhende.
Kipindi hicho cha kwanza Yanga walifika mara kadhaa langoni kwa Komorozine, lakini Hamisi Kiiza, Ngassa, Simon Msuva na Haruna Niyonzima walishindwa kutumia vyema nafasi walizozipata, huku Wacomoro wenyewe wakishindwa kufanya mashambulizi ya hatari.

Yanga walibadilika kipindi cha pili na kufanya mashambulizi yalizaa mabao ya haraka haraka yaliyofungwa na Didier Kavumbagu dakika ya 57 kabla ya Hamisi Kiiza kufunga la nne dakika ya 59.

Ngassa alifunga mabao mawili ya haraka haraka dakika za 64 na 68 hivyo kupiga hat-trick jana, wakati bao la saba lilifungwa na Kavumbagu dakika ya 80.
Wacomoro hawakufanya mashambulizi ya nguvu, hivyo kumfanya kipa Juma Kaseja wa Yanga kutokuwa na kazi kubwa.

Matokeo ya mchezo huo yamedhihirisha ubabe wa Yanga kwa timu za Comoro, ambayo haina historia nzuri katika soka kimataifa.
Komorozine inakuwa timu ya tatu kukutana na Yanga kwenye michuano ya Afrika baada ya AJSM na Etoile d'Or Mirontsy.

Januari 27, mwaka 2007 katika Ligi ya Mabingwa Afrika, raundi ya awali Yanga iliifunga AJSM mabao 5-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na moja kwa moja kufuzu Raundi ya Kwanza, kwa sababu hakukuwa na mchezo wa marudiano kwa kuwa Comoro hawakuwa na Uwanja wenye kukidhi sifa za michuano ya Afrika.

Mwaka 2009, Yanga iliitoa timu nyingine ya Comoro, Etoile de Mironsty kwa jumla ya mabao 14-1, ikianza kushinda 8-1 Januari 31 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kushinda 6-0 ugenini, wakati huo ikiwa chini ya kocha Mserbia, Dusan Kondic.

Hata hivyo mbio za Yanga ziliisha baada ya kutolewa na mabingwa wa kihistoria Afrika, Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 4-0, ikianza kufungwa 3-0 Machi 15 mjini Cairo  na baadaye 1-0 wiki mbili baadaye Dar es Salaam.

Kutokana na matokeo hao Yanga sasa wanahitaji ushindi wowote, sare ama wasifungwe zaidi ya mabao 7-0 ili waingie raundi inayofuata, ambapo watacheza na Ahly , ambao ndio mabingwa watetezi wa Afrika.

Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub, Kevin Yondan/Rajab Zahir, Frank Domayo, Simon Msuva/Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza, Mrisho Ngassa na David Luhende/Didier Kavumbangu.

Komorozine; Attoumani Farid, Ali Mohamed Mouhousoune, Nizar Amir, Abdou Moussoidi Kou, Ahamadi Houmadi Ali, Moidjie Ali, Mourthadhoi Fayssol, Attoumane Omar, Mohamed Erfeda/Imroina Ismael dk30, Mouyade Almansour Nafouondi na Ahmed Waladi Mouhamdi/Ghaidane Mahmoud dk80.


No comments:

Post a Comment