Pages

Saturday, January 25, 2014

YANGA YAENDELEA KUKAA KILELE BAADA YA KUIFUNGA ASHANTI UNITED 2-1 TAIFA




TIMU ya Yanga  imeonesha matunda ya kambi yake iliyopiga Uturuki baada ya kuanza vizuri mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania bara kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ashanti United, mchezo uliopigwa dimba la taifa jijini Dar es Salaam.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu katika dakika ya 61 na David Luhende katika dakika ya 80.

Katika mchezo huo, kipindi cha kwanza timu zote zilikosa nafasi nyingi za wazi za kufunga, huku Yanga ikipoteza nafasi tatu kupitia kwa Kavumbagu, Said Bahanuzi na Mrisho Ngassa.

Kwani Kavumbagu alibaki yeye na kipa na akataka kumpiga chenga, lakini kipa, Daudi Mwasonge aliweza kuokoa hatari hiyo.

Nao Ashanti walionekana kuchangamka, huku mchezaji wake, Bright Obinna akipoteza nafasi ya wazi ya kufunga baada ya kumpiga chenga, Juma Abdul beki wa kulia wa Yanga.

Dakika ya 37 Yanga ilimtoa Bahanuzi na nafasi yake kuchukuliwa na Saimon Msuva na Haruna Niyonzima alikosa nafasi ya wazi ya kufunga eneo la hatari baada ya shuti kale kupaa.

Dakika ya 44, Husen Sued wa Ashanti alikosa nafasi ya wazi kutokana na uimara wa kipa wa Yanga. Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilitoshana nguvu.

Kipindi cha pili Yanga walikianza kwa kasi na walifanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya 52 likifungwa na Kavumbagu akiunganisha pasi ya Simon Msuva.

Mara baada ya kuingia kwa bao hilo, Ashanti walijitahidi kulishambulia lango la Yanga na wakapata bao la kusawazisha dakika ya 61 likifungwa na Obinna aliyemalizia kazi nzuri ya Hussen Sued.

Wakati mchezo huo ukitazamiwa kumalizika kwa sare ya bao 1-1, David Luhende akaifunga Yanga bao la pili katika dakika ya 80 na kuihakikishia pointi zote tatu.

Kwa matokeo hayo sasa Yanga inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi kuu kwa kujikusanyia pointi 31 baada ya kushuka dimbani mara 14.

Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbangu/Hussein Javu, Said Bahanuzi/Simon Msuva na David Luhende.

Ashanti United; Daudi Mwasongwe, Hussein Mkongo, Abdul Mtiro, Shaffi Hassan, Tumba Swedi, Mohammed Fakhi, Abdul Manani/Iddi Suleiman, Fakih Hakika, Bright Obinna/Paul Maona, Hussein Swedi na Joseph Mahundi na Deogratias Munish "Dida".

No comments:

Post a Comment