Pages

Saturday, January 4, 2014

ASHANTI UNITED YATOKA SARE NA SPICE STARS HUKU MBEYA CITY IKICHEZEA KICHAPO TOKA KWA CLOVE STARS

Na Mahmoud Zubeiry, Zanzibar
ASHANTI United na Mbeya City zimejiweka pagumu katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, baada ya jioni hii kupata matokeo yasiyofurahisha katika viwanja viwili tofauti visiwani Zanzibar.
Wakati Ashanti United inayofundishwa na kocha mkongwe Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ imetoa sare ya 1-1 na Spice Stars Uwanja wa Amaan, Unguja, Mbeya City ya Juma Mwambusi imefungwa mabao 2-1 na Clove Stars Uwanja wa Gombani, Pemba.   
Beki wa Spice Stars,Said Ahmed kushoto akiupitia mpira miguuni mwa mshambuliaji wa Ashanti United, Kassim Kilungo jioni hii Uwanja wa Amaan

Huu ni mchezo wa kwanza Mbeya City inafungwa tangu ipande Ligi Kuu.
Uwanja wa Amaan, Ashanti ilitangulia kupata bao kupitia kwa Mnigeria, Ekee Brayton Oina dakika ya 21 katika mchezo wa Kundi C, kabla ya Abdillah Seif Bausi kuisawazishia Spice dakika ya 70.
Uwanja wa Gombani, Paul Nonga alitangulia kuifungia Mbeya City dakika ya tisa katika mchezo wa Kundi A, lakini Mwinyi Mngwali akaisawazishia Chuoni dakika ya 41 kabla ya George Thomas Mkoba kufunga la ushindi dakika ya 64.
Katika mchezo uliotangulia Saa 8:00 mchana wa Kundi A Gombani, URA ya Uganda iliitandika mabao 3-1 Clove Stars ya Pemba. Mabao ya URA yamefungwa na Owen Kasuule na Thery Ali mawili, wakati bao la Clove lilifungwa na Ahmed Ali Omar.
Kwa matokeo hayo, Ashanti inakuwa na pointi moja baada ya kucheza mechi mbili, hivyo inalazimika kushinda mchezo wa mwisho dhidi ya Azam FC keshokutwa ili kuweka matumaini ya kwenda Robo Fainali. 
Kwa Mbeya City nayo ina pointi moja baada ya kucheza mbili na sasa inalazimika kushinda mechi ya mwisho dhidi ya URA ili kuweka hai matumaini ya kwenda Robo Fainali.

No comments:

Post a Comment