Uongozi wa
klabu ya Young Africans SC umempatia taarifa (Notice) ya siku ya
thelathini (30) kocha mkuu mholanzi Ernie Brandts juu ya kusitisha
mkataba wake kuanzia jana Disemba 22 mwaka huu.
Maamuzi hayo yanafuatia muenendo wa matokeo mabaya
katika michezo iliyopita ya Ligi Kuu, kirafiki na bonanza la Nani Mtani
Jembe dhidi ya Simba SC mwishoni mwa wiki.
Hatua
ya Young Africans SC kusitisha huduma na Brandts isichukuliwe kama chuki
bali ni moja ya sehemu ya kuhakikisha tunaboresha benchi la ufundi ili
tuweze kupata matokeo mazuri katika Mashindano yanayotukabili.
Ukitazama
uwezo wa mchezaji mmoja mmoja wa Yanga SC na wapinzani wetu, na soka
tulilocheza kwenye mchezo wa mwishoni mwa wiki kwa kweli ni dhahiri
mwalimu amefikia mwisho kimbinu na hana njia mbadala.
Young
Africans SC imekua ikicheza chini ya kiwango katika michezo ya Ligi Kuu
hali iliyoplekea kupata ushindi kwa tabu na wakati mwingine timu
kupoteza pointi.
Kufuatia kupewa taarifa ya siku
30, Brandts ataamua mwenyewe kama ataendelea kusimamia mazoezi ya timu
au kuondoka moja kwa moja kabla ya muda huo ukiwa haujakamilika.
Ikiwa
Brandts ataondoka mapema timu itaendelea na mazoezi kama kawaida katika
kila siku asubuhi katika uwanja wa bora kijitonyama kujiandaa na
mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa chini ya kocha
msaidizi Fred Felix “Minziro”.
Ili kuhakikisha
timu inafanya vizuri katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom na
mashindano ya kimataifa uongozi unakamilisha maandalizi ya safari ya
kambi nje ya nchi na taratibu zote zitakapokamilika tutawajulisha.
Aidha
uongozi upo katika mchakato wa kumapata mrithi wa Brandts ambaye
ataungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya mzunguko wa pili na
Mashindano ya klabu Bingwa Afrika.
Mwisho
tunawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa Yanga wasivunjike moyo
kufuatia matokeo ya bonanza mwishoni mwa wiki, uongozi unajipanga
kuhakikisha timu inaimarika kwenye benchi la ufundi na kurudisha furaha
katika mzunguko wa pili wa VPL.
Abdallah Bin Kleb
Mwenyekiti - Kamati ya Mashindano
Young Africans Sports Club.
No comments:
Post a Comment