Na Mahmoud Zubeiry, Mombasa
ROBO Fainali za kwanza za Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Chalenge zinatarajiwa kuchezwa leo Uwanja wa Manispaa, Mombasa, Kenya.
Mechi inayotarajiwa kuteka hisia za wengi ni kati ya mabingwa watetezi, Uganda The Cranes dhidi ya Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars itakayoanza saa 8:00 mchana, ingawa kutakuwa na mchezo mwingine kati ya Kenya na Rwanda saa 10:00 jioni.
REKODI YA BARA NA UGANDA CHELLENGE TANGU 1973…
Sept. 29, 1973;
Uganda 2-1 Tanzania, Fainali
Sept. 25, 1974
Tanzania 1-1 Uganda(Bara ilishinda penalti 5-3 fainali)
Nov. 9, 1979
Tanzania 5 – 3 Uganda Kundi A
Nov. 17, 1982
Uganda 1 – 0 Tanzania Kundi A
Des. 1, 1984
Uganda 1 – 1 Tanzania Kundi A
Des. 8, 1989
Uganda 5 – 1 Tanzania Kundi A
Des. 17, 1990
Uganda 1-1 Tanzania (Uganda ilishinda penalti 6-5 Nusu Fainali)
Nov. 30, 1991
Uganda 5 – 0 Tanzania Kundi A
Nov. 28, 1992
Uganda 1 – 0 Tanzania B ‘Kakakuona’, Fainali
Des. 10, 1994
Tanzania 2-2 Uganda (Bara ilishinda penalti 4-3 fainali) Nov. 22, 1996
Uganda 1 – 0 Tanzania Kundi A
Des. 11, 2001
Tanzania 1 - 0 Uganda Kundi B
JanuarI 9, 2008
Uganda 2 - 1 Tanzania Kundi A
Nov. 29, 2009
Tanzania 0-2 Uganda Kundi C
Des. 10, 2010
Uganda 0 – 0 Tanzania (Bara ilishinda penalti 5-4 Nusu Fainali
Des. 8, 2011
Uganda 3-1 Tanzania (Nusu Fainali dakika 120)
Des 6, 2012
Tanzania 0–3 Uganda (Nusu Fainali)
Des 7, 2013;
Tanzania Vs Uganda, Nusu Fainali
Stars wanaingia katika sura ya unyonge kumenyana na The Cranes inayofundishwa na kocha hodari Afrika, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’ kutokana na kufungwa mfululizo na wapinzani wao hao siku za karibuni.
Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayoundwa na idadi kubwa ya wachezaji wa Bara ilifungwa nyumbani na ugenini na Uganda katika mechi za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za CHAN.
Lakini pia, Uganda imeonyesha ni tishio katika Challenge ya mwaka huu baada ya kufuzu Robo Fainali kwa kushinda mechi zake zote za Kundi C, wakati Bara ilipata ushindi mwembamba wa 1-0 mara mbili na sare moja hivyo kushika nafasi ya pili Kundi B.
Kocha Mdenmark, Kim Poulsen amesema kwamba anawaheshimu Uganda ni timu nzuri na anatarajia mchezo utakuwa mgumu, lakini yeye amewaandaa vyema vijana wake kushinda mechi ya leo.
Micho pia amesema Stars ni wazuri hasa baada ya kuwasili kwa washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu ambao amesema wakiungana na Mrisho Ngassa watetengeneza safu kali ya ushambuliaji.
Kwa ujumla makocha wote wanaogopana kuelekea mchezo huo- jambo ambalo linaashiria hiyo ni mechi isiyotabirika hata chembe.
Kama alivyosema Micho, safu ya ushambuliaji ya Stars leo inatarajiwa kuongozwa na Ngassa, Ulimwengu na Samatta wakati viungo wanaweza kuwa Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Athumani Iddi ‘Chuji’.
Langoni ataanza Ivo Mapunda, kulia Himid Mao, kushoto Erasto Nyoni na katikati Said Morad na Kevin Yondan.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Uganda, Emanuel Okwi, Hamisi Kiiza na Dani Sserunkuma wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji, wakati wengine kikosini watakuwa Nico Wadada, Godfrey Kizito, Khalid Aucho, Brian Majwega, Vincent Kayizzi, Godfrey Walusimbi, Savio Kabugo na Benjamin Ochan langoni.
Emmanuel Okwi ndiye tegemeo la mabao la Uganda Challenge |
Kenya inapewa nafasi kubwa ya kuitoa Rwanda katika mchezo wa pili. Je, Stars itafuta uteja kwa The Cranes leo?
Kwa hisani ya Bin Zubeiry
No comments:
Post a Comment