Pages

Wednesday, November 6, 2013

SIMBA YAFUNGA PAZIA LA MZUNGUKO WA KWANZA KWA KUIFUNGA ASHANTI UTD 4-2 LEO TAIFA

Mshambuliaji wa Simba Betram Mwombeki (katikati) akishangilia bao lake la pili kwenye mchezo  wa Ligi Kuu dhidi ya Ashanti United leo. Kushoto ni Ramadhan Singano ma kulia ni Amis Tambwe ambaye leo amefikisha mabao 10 




Wachezaji wa Simba wakishangilia bao lao la kwanza lililofungwa  na Ramadhan Singano
SIMBA leo imewafariji mashabiki wake baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 4-2 katika mchezo wa mwisho wa duru la kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.
Ushindi huo angalau umewapa furaha mashabiki wa timu hiyo kutokana na matokeo yasiyoridhisha katika michezo kadhaa iliyopita na hivyo kusababisha benchi la ufundi la timu hiyo kuwa katika shinikizo kubwa kutoka kwa mashabiki.
Hata hivyo, licha ya ushindi huo, Simba bado ipo nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 24 nyuma ya Yanga yenye pointi 25 ikiwa nafasi ya tatu, Mbeya City yenye pointi 26 na Azam inayoongoza ikiwa pia na pointi 26.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo, ambapo Uwanja wa Taifa Yanga itacheza na JKT Oljoro, huku Uwanja wa Azam, Mbeya City itakuwa mgeni wa Azam.
Katika mchezo wa jana, Simba ilipata bao la kwanza dakika ya nane mfungaji akiwa Ramadhani Singano ‘Messi’ kutokana na pasi ndefu ya Jonas Mkude.
Ashanti ilionekana kutawala zaidi kipindi cha kwanza, ambapo mara kadhaa ilifika kwneye lango la Simba lakini umaliziaji haukuwa mzuri.
Dakika ya 31 Said Maulid ‘SMG’ angeweza kuiandikia bao Ashanti, lakini alishikwa na kigugumizi cha miguu alipokuwa karibu na lango la wapinzani wao.
Ashanti ilipata bao la kusawazisha dakika ya 45 mfungaji akiwa Hussein Sued kwa kichwa kutokana na krosi ya Hussein Mkongo.
Mrundi Amisi Tambwe aliiandikia Simba bao la pili likiwa ni bao lake la kumi msimu huu, dakika moja tangu kuanza kipindi cha pili, baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Singano.
Simba ilifanya mabadiliko, ambapo William Lucian na Said Ndemla waliingia  kuchukua nafasi za Henry Joseph na Amri Kiemba, mabadiliko yaliyoonekana kuiimarisha zaidi timu hiyo.
Dakika ya 50 Betram Mwombeki alifunga bao la tatu akimalizia pasi ya Haruna Shamte aliyegongeana vyema na Singano.
Maulid ambaye aliwahi kuichezea Simba kabla ya kwenda Angola kucheza soka la kulipwa, aliifungia Ashanti United bao la pili dakika ya 53 akimalizia kazi nzuri ya Paulo Maona. Dakika ya 61 Mombeki alifunga bao kwa kichwa akiunganisha wavuni krosi ya Haruna Shamte.
Simba: Abuu Hashimu, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Gilbert Kaze, Hassan Hatibu, Jonas Mkude, Ramadhani Singano ‘Messi’, Henry Joseph, Betram Mombeki, Amisi Tambwe na Amri Kiemba.
Ashanti: Amani Simba, Hussein Mkongo, Jafari Gonga, Tumba Sued, Samir Ruhava, Idd Said, Fakhi Hakika, Paul Maona, Hussein Sued, Said Maulid na Joseph Mahundi.

Wakati huohuo, JKT Ruvu jana iliifunga Coastal Union bao 1-0 katika mchezo mwingine wa ligi hiyo uliofanyika Uwanja wa Azam Chamazi, ambapo bao la washindi lilifungwa na Bakari Kondo.

No comments:

Post a Comment