Pages

Tuesday, November 12, 2013

HASANOO ASHINDA KESI YA SHABA, ARUDISHWA TENA MAGEREZA KWA KESI YA KUHUJUMU UCHUMI

MAHAKAMA  ya Hakimu Mkazi Kisutu imemuachia huru Katibu Mkuu wa zamani wa klabu ya Simba, Hassani Othman ‘Hasanoo’ na wenzake wawili baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka ya wizi wa Shaba za Sh milioni 400.

Hata hivyo baada ya kusomwa kwa hukumu hiyo Hassanoo alirudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na kesi nyingine ya uhujumu uchumi.

Hukumu hiyo ilisomwa jana mahakama hapo na Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, baada ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka aliyetakiwa kusoma hukumu hiyo kutokuwepo.
Hakimu Fimbo alisema katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na mashahidi 13 wa upande wa mashitaka haujathibitisha kuwa washitakiwa hao walikula njama au kuwasiliana kwa kupanga kutenda kosa hilo kwa njia yoyote.

Aidha alisema hakuna shahidi aliyethibitisha kuwa madini hayo yaliibiwa na awali upande wa  mashitaka ulileta washitakiwa wanne na baadaye mmoja kuondolewa, lakini ilishangaza kuona mtu huyo hakuitwa mahakamani kutoa ushahidi.

Katika mashitaka ya kupatikana na mali iliyoibiwa, Hakimu Fimbo alisema hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa washitakiwa hao waliiba au kupokea shaba hizo.
"Kulingana na ushahidi uliotolewa mahakamani, washitakiwa hawana hatia na wote nawaachia huru," alisema Hakimu Fimbo.

Mbali na Hassanoo, washitakiwa wengine ni Wambura Mahenga ambaye ni mshitakiwa wa kwanza na Dk Najim Msenga ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa madini na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi taifa (NEC).

Washitakiwa hao walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu, ambapo wanadaiwa Agosti 26, mwaka huu walikula njama  ya kutenda kosa la kuiba vitu vilivyokuwa vikisafirishwa.
Kosa la pili ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, washtakiwa hao waliiba shaba hiyo mali ya Kampuni ya Libert Express(T)Limited iliyokuwa ikisafirishwa na lori T 821 ABC lililokuwa na tela T 566 BCZ likitokea Zambia.

Katika kosa la tatu ilidaiwa kuwa, watuhumiwa hao walipokea  shaba hizo huku wakijua kuwa,  mali hizo zimepatikana kwa njia isiyo halali.


Akizungumza nje ya Mahakama baada ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Dk Msenga alisema kuwa hukumu hiyo imetolewa kwa kuzingati haki, kutokana na ukweli ulioelezwa mahakamani hapo.

No comments:

Post a Comment