Pages

Monday, November 25, 2013

DAKTARI WA TAIFA STARS MWANANDI MWANKEMWA KUSTAAFU KAZI, NAFASI YAKE KUCHUKULIWA NA KAPINGA

Mwankemwa akiwa pamoja na timu ya taifa

DAKTARI Mkuu wa timu ya Taifa, ‘Taifa stars’ Mwanandi Mwankemwa anatarajia kustaafu kuitumikia timu hiyo mara baada ya kumalizika mashindano ya Kombe la Chalenji yanayotarajiwa kesho jijini Nairobi, Kenya.

Akizungumza na Spoti Leo, wakati wa mazoezi ya Taifa stars yaliyofanyika Karume jana, Mwankemwa alisema kuwa ameamua kustaafu kwa sababu ya tatu, moja ni kuongezeka kwa majukumu, pili ni Mwenyekiti wa Chama cha Madaktari pia mjumbe wa kamati ya tiba ambayo ipo chini ya shirikisho la soka nchini (TFF).

“Kweli mimi nimeona ni busara kuachia majukumu kwa wengine kwani nina majukumu mengi na mengine yananitaka nitoe maelekezo kwa ninaowaongoza na ikumbukwe kuwa mimi pia nina ajira ambayo nahitajika kuitumikia”, alisema Mwankemwa.

Pia alisema kuwa yeye alitarajia ule mchezo wa Taifa Stars na Zimbabwe ndio ungekuwa wa mwisho kwake kuwepo kwenye benchi la Taifa stars ndio maana alipiga picha na kikosi hicho lakini Kim Poulsen aliomba aendelee hadi mashindano ya Chalenji yatakapomalizika.

Habari ambazo Spoti Leo imezipata nafasi ya Mwankemwa itachukuliwa na daktari Cosmas Kapinga ambaye alikuwa dakatari wa timu ya Simba kwa msimu uliopita.
Mwankemwa alisema alianza kujihusisha na tiba ya uanamichezo mwaka 1982, baada ya kuumia goti na kushindwa kucheza mpira kwani alikuwa akiichezea Ruvu stars na daadae alihamishiwa kikazi hospitali ya Temeke na kuendelea kutibu timu za shule katika mashindano mbalimbali.

Mwaka 1984 hadi 1989 alikuwa anatibu timu za Redstars na Panafrika, vilevile aliwahi kuwa daktari wa timu ya Vijana ya mkoa Dar es Salaam ‘Mzizma United’.
Alianza kutibu Taifa Stars 2006, na anasema kuwa kocha mkuu wa wakati huo Mshindo Msola ndiye aliyempendekeza enzi za FAT lakini alipokuja kocha Marcio Maximo alishindwa kuwepo kwenye benchi la Ufundi la timu hiyo kutokana na ajali ya gari aliyopata na kulazimika kupumzika kwa miaka miwili.

Baada ya kuja Jan Poulsen Mwanakemwa alirudi kuendelea kuitumia Taifa stars hadi sasa ambapo ipo chini ya kocha Kim Poulsen.
Mwankemwa ambaye pia ni dakatari wa timu ya Azam vileviele ni Mwenyekiti wa bodi ya olimpiki maalum.


Katika kazi yoyote kuna mafanikio, hivyo anajivunia Kilimanjaro Stars ilipotwaa kombe la Afrika Mashariki na Kati akiwa na kocha Jan Poulsen 2010 lakini pia nasema hatasahau kipindi timu ya Taifa ya Vijana ilipogomea mchezo dhidi ya Nigeria wakiwa ugenini enzi za FAT na yeye kuhusishwa na mgomo huo jambo ambalo anasema haikuwa kweli kwani wachezaji walikuwa wanadai posho zao lakini uongozi wa akina Ndolanga kwa kuficha udhaifu wao wakamsingizia yeye.

No comments:

Post a Comment