Pages

Friday, October 25, 2013

NYAMLANI ATANGAZA VIPAUMBELE TISA ATAKAVYOSHUGHULIKIA ENDAPO ATAINGIA TFF



 
MGOMBEA wa nafasi ya Urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Athman Nyamlani ametaja vipaumbele tisa vya maendeleo ya soka, iwapo atapata ridhaa ya wapiga kura kuliongoza Shirikisho hilo.




Akizungumza Dar es Salaam jana katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi utakaofanyika Jumapili, Nyamlani alisema akipewa nafasi hiyo, atainua kiwango cha soka  kwa kuimarisha usimamizi wa menejimenti ya soka katika ngazi zote.




Nyamlani  ambaye ni Makamu wa Rais anayemaliza muda wake alisema endapo atapata ridhaa ya wapiga kura kuliongoza shirikisho hilo  pia atahakikisha kunakuwepo na mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi na kusimamia sheria na taratibu za uendeshaji wa soka la Tanzania na suala la viongozi  kujiendeleza kielimu litapewa kipaumbele na litakuwa ni agenda endelevu.
Alisema kuwa kama atakuchagulia pia atapambana na vitendo vya rushwa katika soka kwa kuwa vimekuwa kikwazo kikubwa katika upatikanaji wa maendeleo endelevu ya mchezo huo.

“Naomba nikiri kuwa kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka, wachezaji, waamuzi na wadau wengine. Hivyo basi kwa kushirikiana na serikali na viongozi wa soka katika ngazi zote nitahakikisha naendeleza mapambano dhidi ya rushwa katika mchezo soka, kuanzia katika ngazi za uongozi na soka la viwanjani,” alisema.

Alisema kipaumbele cha tatu kitakuwa ni kukuza soka la watoto, vijana na wanawake,  na kwamba akiwa kama Rais wa TFF, atalipa uzito wa kipekee soka la watoto wenye umri wa miaka chini ya 16 na soka la vijana na kukuza vipaji kuanzia miaka tisa hadi 21 na soka ya wanawake.

Nyamlani alisema kazi hiyo ataitekeleza kwa kuanzisha program mbali za mashindano na za kukuza vipaji kwa makundi haya ya vijana kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa soka.

“Katika uongozi unaomaliza muda wake tumejitahidi sana kuyasukuma makundi haya na yameonyesha mwanga, hivyo nikishika wadhifa kama Rais nitaendeleza programu hizi kwa  kushirikiana na viongozi wa soka katika ngazi mbalimbali na serikali,” alisema.

Kipumbele kingine muhimu ni Kuimarisha Uwezo wa Rasilimali Fedha wa Shirikisho, kama Rais wa TFF atahakikisha kuwa TFF inapata vyanzo endelevu na vya kuaminika ili kuweza kujenga uwezo wa shirikisho katika kutekeleza mipango kikamilifu.

No comments:

Post a Comment