Pages

Wednesday, September 4, 2013

WACHEZAJI SIMBA WAFUNGIWA LUKU



SIMBA imekuja na mfumo mpya wa mazoezi, uliobatizwa jina la 'Simba Luku', ambao una lengo la kuwafanya wachezaji kuongeza bidii ya mazoezi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' ndiye aliyeubuni mfumo huo, akiufananisha na mita za Luku, ambazo mtumiaji hulipia umeme kadri anavyotumia.

Julio anamaanisha kwamba kuanzia sasa wachezaji wanatakiwa kujituma zaidi ili walipwe posho nzuri zaidi na kuweza kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Kocha Mkuu wa Simba, Abdallah Kibaden, amelifafanua kwamba kwa kupitia mfumo huo, kikosi cha vijana wake kinaweza kuwa na ushindani mkubwa wa namba, kwani kila safu ina wachezaji zaidi ya watatu wanaochuana.

Kwa mujibu wa Kibadeni, mchezaji anatakiwa kujituma vilivyo ili aweze kujihakikishia namba na maslahi zaidi.
"Hilo jina halijakosewa kabisa, maana ushindani uliopo katika kikosi changu ni mkubwa, kama ilivyo kwa mita za Luku, huwezi kupata umeme hadi uingize fedha na hivi ndivyo itakavyokuwa kwa wachezaji wetu, kwani hawataweza kupata nafasi hadi wajitume zaidi mazoezini," alisema Kibadeni.

Kibadeni pia amesema kwamba ameongeza zaidi dozi ya mazoezi kwa vijana wake, ambapo sasa timu itakuwa ikijifua mara mbili, asubuhi na jioni.

Tangu ianze mazoezi juzi Jumatatu, ilikuwa ikifanya mazoezi mara moja kwenye Uwanja wa Kinesi, jijini Dar es Salaam, lakini kuanzia leo Jumatano, Kibadeni ameamua kuwaongezea dozi wachezaji wake.

Kibadeni amelazimika kuongeza mazoezi kutokana na kuweka nia ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu na kuijenga timu kwa stamina zaidi.
Akizungumzia maandalizi yake ya mechi dhidi ya Mtibwa Sugar, itakayochezwa Septemba 14 mwaka huu, Kibadeni alisema kwamba hawezi kuanika mbinu atakazotumia, lakini kwa jinsi timu yake ilivyojipanga anaamini watashinda.

No comments:

Post a Comment