Pages

Monday, September 2, 2013

SIMBA YAWAFUNZA MAFUNZO SOKA TAIFA, TAMBWE ATUPIA MBILI



UWEZO wa mshambuliaji wa kimataifa wa Simba, Amis Tambwe kutoka Burundi, huwezi kuupimisha na mchezaji yeyote wa kimataifa kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya soka ya Vodacom Tanzania Bara.

Nyota huyo jana alifunga mabao mawili katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar na kuiwezesha Simba kupata ushindi wa mabao 4-3 kwenye mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tambwe, hadi sasa ameifungia Simba mabao matatu katika mechi tatu alizoichezea timu hiyo na ametoa usaidizi wa mabao manne likiwemo moja katika mchezo wa jana wa kirafiki. Hali hiyo inaonyesha wazi kwamba mshambuliaji huyo ni chaguo sahihi na kwamba Simba sasa imepata muarobaini wa mabao, baada ya kuondoka kwa aliyekuwa mshambuliaji wake tegemeo, Emmanuel Okwi.

Katika mechi hiyo ya kirafiki, kila upande ulianza kwa kufanya mashambulizi huku Mafunzo wakionekana kutawala zaidi nafasi ya kiungo, hali iliyowafanya kusukuma zaidi mashambulizi langoni mwa Simba na hatimaye walifanikiwa kupata bao katika dakika ya 32, likifungwa na Abdul Abdallah.

Abdul alipiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja kimiani, kufuatia beki wa Simba, Mraji Adam kumfanyia madhambi, Masoud Hamad nje kidogo ya eneo la hatari.

Bao hili liliwafanya Simba kuja juu na kuliandama lango la Mafunzo, lakini washambuliaji wake hawakuwa makini, hiyo iliwalazimu kusubiri hadi dakika ya 45 kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Amis Tambwe akimalizia krosi ya Rashid Ismail na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa sare ya 1-1.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko, ambapo Simba walionekana kuimarika na kunufaika na mabadiliko hayo, baada ya kupata bao dakika ya 47, lililofungwa na Sino Agustino  aliyeingia kuchukua nafasi ya Rashid Ismail. Sino aliunganisha krosi ya Tambwe.

Hata hivyo, Mafunzo walikuja juu na kusawazisha dakika ya 52 kwa bao lililofungwa na  Jaku Joma, baada ya mabeki wa Simba kumdharau kisha mshambuliaji huyo kuachia shuti kali lililomshinda kipa, Adrew Ntara wa Simba na kujaa kimiani.

Simba walionekana kupoteana  na kuruhusu Mafunzo kucheza mchezo safi, uliowaamsha mashabiki wa Yanga kuanza kuwashangilia na walifanikiwa kupata bao la tatu katika dakika ya 72 likifungwa na Jaku Othman aliyemalizia krosi ya Henri Salum.

Simba walikuja juu na kusawazisha bao hilo kupitia kwa Tambwe katika dakika ya 81, akiunganisha krosi ya Nasor Masoud ‘Chollo’ na dakika mbili baadaye, Chollo aliwainua mashabiki wa Simba kwa bao safi baada ya kuunganisha krosi ya Singano.
 
Hamis Tambwe akishangilia bao aliloifungia timu yake.



Mshambuliaji wa Simba, Hamis Tambwe (kulia) akitafuta mbinu za kumtoka beki wa Mafunzo, Jumbe Omari Jumbe katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Hekaheka katika lango la Mafunzo.

Beki wa Mafunzo Ali Vuai Juma (kushoto) akichuana na mshambuliaji mpya wa Simba kutoka Burundi, Hamis Tambwe katika mchezo wa kirafiki uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Beki wa Mafunzo, Jumbe Omar Jumbe akimdhibiti mshambuliaji wa Simba, Hamis Tambwe.

Golikipa wa timu ya Mafunzo ya Unguja, Ussi Makame Ussi akiwa hana la kufanya baada ya kushindwa kuzuia kiki iliyopigwa na mshambuliaji wa Simba, Hamis Tambwe (kushoto) na kuipatia timu yake bao la kwanza katika mchezo wa kirafiki uliofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam. (Picha na Francis Dande)

Golikipa wa Mafunzo, Ussi Makame Ussi akiruka bila mafanikio kujaribu kuokoa mpira uliopigwa na mshambuliaji wa Simba, Hamis Tambwe na kuhesabu bao la kwanza kwa timu yake

No comments:

Post a Comment