Pages

Sunday, September 1, 2013

SIMBA YAJIZATITI KUFANYA VIZURI LIGI KUU



SIMBA imetangaza kiama kwa timu za Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, baada ya kikosi chake kufanya mazoezi kwa pamoja na wachezaji walioongezwa kikosini.

Wekundu hao wa Msimbazi, wikiendi iliyopita walianza ligi vibaya kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Rhino ya Tabora, huku wapinzani wao, Yanga wakichekelea ushindi wa mabao yao 5-1 dhidi ya Ashanti United, lakini Jumatano iliyopita hali ikawa ni tofauti kwa Simba kushinda bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro na Yanga kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Ashanti United.

Sasa timu hizo mbili zinalingana kwa pointi, lakini kocha wa Simba, Abdallah Kibadeni amesema wataanza ligi katika mechi ijayo.
Katika mechi zijazo ambazo ni za mzunguko wa tatu zitakazopigwa kwenye viwanja tofauti, Simba SC watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Coastal Union wataikaribisha Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Ruvu Shootings watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT Uwanja wa Mabatini, Pwani, JKT Oljoro wataikaribisha Rhino Rangers Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha, Mbeya City wataikaribisha Yanga SC Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Kaitaba, Kagera, wakati Ashanti United watamenyana na JKT Ruvu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam. 

Kibadeni aliliambia DIMBA kwamba kilichowafanya waanze ligi kwa kusuasua ni kuvurugwa kwa mipango yake, ambapo walijikuta wakipewa taarifa za kushtukiza kwamba hawatakiwi kuwatumia wachezaji wa kigeni, Hamis Tambwe na Kaze Gilbert, ambao walikuwa kwenye mipango yake.

"Kusema kweli taarifa ile ilitushtua, tulitegemea kuwatumia lakini hatukuweza kutokana na kushtukizwa, hivyo mimi kama kocha, nililazimika kupanga kikosi ambacho sikukitarajia," alisema Kibadeni.
Alisema hata katika mchezo dhidi ya JKT Oljoro walipotoka sare ya bao 1-0, aliwapanga kina Kaze lakini kutokana na ugeni wao kwenye kikosi, ndio maana waliibuka na ushindi mwembamba.

Hata hivyo alisema kwa hivi sasa wamerudi kwenye mstari, huku kikosi cha timu hiyo kikiongezwa nguvu na ujio wa kiungo wa zamani Henry Joseph, ambaye jana alikuwepo kwenye mazoezi kwenye uwanja wa Kinesi, hivyo kumpa matumaini kocha huyo ya kufanya vizuri kwenye ligi.

Kwa sasa ligi hiyo inakwenda mapumziko kwa wiki mbili, baada ya raundi mbili za awali, kupisha maandalizi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ya mchezo wa mwisho wa kufuzu Kombe la Dunia mwakani Brazil, dhidi ya Gambia, Septemba 7, mwaka huu.  

Baada ya kila timu kucheza mechi mbili, JKT Ruvu ipo kileleni kwa pointi zake sita na mabao matano kufuatia kushinda mechi mbili ugenini na nyumbani, wakati inaziacha timu za nyuma yake kwa pointi mbili.
Yanga SC, iliyoanza kwa kishindo ikishinda 5-1 dhidi ya Ashanti United, ililazimishwa sare ya 1-1 na Coastal Union, wakati Simba iliyoanza kwa sare ya 2-2 na Rhino mjini Tabora ikizinduka na kushinda 1-0 Arusha.
Azam nayo iliyoanza kwa sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Morogoro, ilizinduka na kuifunga 2-0 Rhino Rangers mjini Tabora. 

Kwa upande wa mabao, mbio za kuwania kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu zinaanzishwa na wachezaji watatu, Jerry Tegete wa Yanga, Bakari Kondo wa JKT Ruvu na Jonas Mkude wa Simba SC, ambao wote kila mmoja ana mabao mawili.
Baada ya mechi mbili za awali, timu zinakwenda kujipanga kabla ya kuendelea na ligi hiyo, Septemba 14, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment