Pages

Thursday, August 29, 2013

CHEKA ATAWAFANYA WATANZANIA WACHEKE LEO?







BONDIA wa ngumi za kulipwa, Francis Cheka, leo anatarajia kumaliza ubishi na mpinzani wake kutoka Marekani, Phil Williams, katika pambano la kuwania ubingwa wa dunia.
Pambano hilo la raundi 12 uzito wa kilogramu 76, litafanyika kwenye Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza wakati wa kupima uzito, Cheka kutoka Morogoro alisema kuwa  atamchapa Mmarekani ili kudhihirisha ubora wake.
“Nimejiandaa vya kutosha na matumaini yangu ni kuendeleza ubabe ili kubakisha mkanda huo nyumbani,” alisema.
Alipoulizwa kama anamjua mpinzani wake, Cheka alisema kuwa hajaona CD za mpinzani wake, ila amejipanga kwa vita.
“Mimi ni bora na nimejipanga vya kutosha, mpinzani wangu nitampiga raundi za mwanzo mwanzo licha ya kutoona CD zake,” alisema Cheka.
Phil Williams alisema ameona video za mpinzani wake na tayari amesoma mbinu anazotumia akiwa kwenye mapambano.
Alisema kuwa ameshinda mapambano 11 yote kwa TKO, hivyo na Cheka ajiandae kwa kichapo hicho hicho.
“Sijawahi kushinda kwa pointi, mapambano yangu yote kwa TKO, hivyo nimeshasoma mbinu za Cheka ajiandae,” alisema.
Katika hatua nyingine, Rais wa WBF, Francois Botha, ambaye aliwahi kuwa bingwa wa dunia  wa uzito wa juu, alitoa kali ya mwaka baada ya kuzigomea ‘gloves’ za waandaaji wa michuano hiyo na kusema kuwa hazina viwango.
Alisema kuwa ‘gloves’ hizo zimechakaa na hazina sifa za kuvaliwa kwenye pambano la kimataifa kama hilo.
“Kwanza zimechakaa halafu zipo chache, zinatakiwa gloves mpya nne kwa ajili ya pambano hilo,” alisema.
Alisema kuwa pambano hilo litakuwa na waamuzi wawili kutoka Afrika Kusini na wawili Tanzania.
Aliwataja waamuzi hao kuwa ni Darryl Rinnoiak, Edward Maeshall wa Afrika Kusini na Fedel Hines, Goha Chagu wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment