Pages

Thursday, June 6, 2013

UJIO WA NEYMAR, HOFU KWA MASHABIKI WA MESSI


MAPENZI ya mashabiki wa Barcelona kwa Lionel Messi, hayafichiki na hayana mwisho na hiyo ndiyo maana usajili wa karibuni wa kinda mchawi wa Kibrazil, Neymar kutoka Santos, umewaacha wakiwa na hofu.

Miamba hiyo ya Catalan imewafunika wapinzani wao, Real Madrid kwa kunasa saini ya Neymar ambaye kwa mujibu wa SportPro, ndiye mwamichezo anayeuzika zaidi duniani kwa sasa.
Unaweza kudhani mashabiki wote wa Barcelona, watakuwa wakishangilia ujio wa Neymar, lakini kiukweli wengi wanahofu.

Wanahofu kwa sababu kuna mengi yako hatarini. Hata kwa wale wasioipenda Barca bado usajili huu unawasisimua, lakini ni rahisi sana kuona wapi mambo yataenda kombo.
Gwiji wa Barcelona, Johan Cruyff aliwahi kunukuliwa akieleza kwa nini Barcelona walikuwa hawajashawishika kumsajili Neymar siku za nyuma.

Alisema: “Ni usajili wa kujivunia na siyo wa kimbinu, ndio maana watu hawana uhakika nao, hasa kutokana na ukweli kuwa Barcelona wanahitaji beki.
“Maswali mengine yaliyozuka ni iwapo Neymar, ambaye amefunga mabao 20 kwenye mechi 32 akiwa Brazil ni mzuri kama anavyoonekana na iwapo ataweza kumudu soka la Ulaya mapema.

“Pia kulikuwa na suala la uwezo wake wa kucheza na Messi, mtu ambaye Barcelona inacheza kwa kumtazama. Messi na Neymar? Manahodha wawili kwenye meli moja hawatafanikiwa.”
Hiyo pointi ya mwisho ya Cruyff, ndiyo itatazamwa sana na makala haya. Ni athari gani zitampata Messi kutokana na ujio wa Neymar? Je, ujio huu utaathiri vipi historia ya Messi Barca kwenye miaka ijayo?
Hatari ya Neymar kumuondoa Messi ni ndogo sana, hasa kwa kipindi kifupi kijacho.

Neymar mwenyewe ameweka wazi kwamba anajua nani ‘kidume’ Barcelona, hii ni kutokana na maneno aliyoandika kwenye tweeter siku aliyotua Barca kuwa atahakikisha anamsaidia Messi kuendelea kuwa bora duniani.
Kama uhusiano kati ya Waamerika Kusini hawa utaendelea kuwa wa bosi (Messi) na kibaraka wake (Neymar) kwenye msimu wa 2013-14, basi miamba hiyo ya Catalan inauwezekano mkubwa sana wa kurudi kileleni kwenye soka la Ulaya, hasa baada ya kudhalilishwa na Bayern Munich karibuni.

Je, itakuwaje kama Mbrazil huyo atashindwa kuendana na soka la Hispania, staili ya Barcelona au kama atashindwa kutimiza ahadi yake ya kucheza chini ya kivuli cha Messi? Barca watafumba macho na kutosa.
Messi ndiye mtawala pande za Camp Nou, katika miaka ya karibuni na hakuna mgeni atakayeweza kumvua utawala huo. Muulizeni Zlatan Ibrahimovic kilichomkuta baada ya kutaka Barcelona wacheze kwa kumtazama yeye.

Iwapo kinda huyo wa zamani wa Santos atafanikiwa kuonyesha ubora wake kwenye miaka ijayo na kuibuka kuwa staa wa Blaugrana, je, ataweza kupata nafasi ya kung’ara kuliko Messi na hatimaye kumpoteza kabisa Barcelona?
Uhusiano wa bosi na kibaraka huwa mzuri pale unapofanya kazi, lakini kumbuka kilichomkuta Obi Wan Kenobi pale kinda Anakin alipochoka kutawaliwa? Hakuna mtu anataka kuuona urithi wa Messi ukipotelea angani. Labda Cristiano Ronaldo atafurahi, lakini hakuna mtu mwingine.

Uwezekano wa nahodha wa Argentina kuondoka Barcelona upo, lakini ni ngumu sana. Anapopata changamoto Messi huachana na zengwe na huwa bora zaidi.
Wanaomponda walisema, Messi huwa hafungi akikutana na miamba ya England, baada ya hapo akafunga mabao manne dhidi ya Arsenal kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wakasema hafungi akiwa na timu ya taifa, lakini chini ya Alejandro Sabella, kila kukicha anaifungia mabao Argentina.

Wakasema kwamba, Ronaldo ndiye mchezaji mwenye kila kitu, lakini Messi amekuwa akimkimbiza kwenye tunzo nne mfululizo za Ballon d'Or. Kila watu wanapohoji ubora wake Muargentina huyo, huwapa majibu yake uwanjani.
Kuna uwezekano mkubwa sana wa Neymar kumfanya Messi kuwa bora zaidi na Messi kumfanya Neymar kuwa bora zaidi. Kijana huyo wa Rosario amekuwa na majukumu makubwa sana Barcelona na iwapo sehemu ya majukumu hayo atapewa mtu mwingine basi Messi atatisha zaidi.

Ubunifu, kujua goli lilipo na akili ya mpira ya hawa wawili ikijumlishwa kwa pamoja basi wanaweza kutengeneza safu ya ushambuliaji bora zaidi kwenye soka kwa miaka 10 au zaidi ijayo.
Iwapo Messi ataendelea kuwa Barcelona kwa miaka minne, sita au 10 ijayo historia itakuwa bora zaidi.

Mafanikio hayo yatakuwa kiama kwa wapinzani wote wa Barcelona, lakini kwa mashabiki wa Lionel Messi, ni sababu ya kufunga mikono pamoja na kutegemea makubwa kuliko kukaa na kujikunyata kwa hofu.

No comments:

Post a Comment