Pages

Thursday, June 6, 2013

JESHI KAMILI LA MOURIHNO HILI HAPA

LONDON, England
HATIMAYE ‘Special One’ amerudi Stamford Bridge kufanya makubwa zaidi, hiyo ni changamoto kwake hasa kutokana na kutwaa mataji sita katika miaka mitatu aliyokaa Chelsea kwenye utawala wake wa kwanza.

Ni vipi Jose Mourinho atafanikiwa katika hilo?
Jibu ni rahisi sana, atafanikiwa kwa kutengeneza uti wa mgongo kwenye timu tena.
Wakati wa utawala wake wa kwanza, alikuwa na Petr Cech golini, John Terry beki wa kati, Frank Lampard kiungo na Didier Drogba mshambuliaji wa kati.
Hawa wote wananjaa ya ushindi, wote ni viongozi na wote ni wachezaji wa mechi kubwa.
Hili linathibitishwa na ubingwa mara mbili wa Ligi Kuu England, mataji mawili ya Kombe la Ligi, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.

Na hii ndiyo sababu itakayomlazimu kutengeneza upya uti wa mgongo wa timu hiyo.
Kikosi cha sasa cha Chelsea kinaubora wa hali ya juu, lakini hakina ari ya ushindi, njaa ya mafanikio pamoja na jihadi kama ilivyokuwa kwenye utawala wa kwanza wa Mourinho.
Na kufanikisha hilo anatakiwa kufanya biashara ya kuuza wachezaji, ili apate fedha za kununua.
Mtu wa kwanza kufunguliwa milango atakuwa Fernando Torres na kuangalia uwezekano wa kumleta Straika wa Napoli, Edinson Cavani kuja kumaliza tatizo la magoli Chelsea.

Mourinho anahaha kutafuta mtu wa kumtazama kwenye safu ya ushambuliaji ya Chelsea, mtu kama Cavani. Lakini pia anaweza kumchukua Robert Lewandowski kutoka Borussia Dortmund au hata Wayne Rooney wa Manchester United.
Bayern Munich wanapewa nafasi ya kumsajili Lewandowski na Man United wanasema Rooney anabaki, kwa hiyo matumaini yote yapo kwa Cavani.
Nyuma ya straika anaweza kutoa nafasi kwa utatu mtakatifu wa Juan Mata, Eden Hazard na Oscar kufanya yao.

Maneno kwamba Mourinho si muumini wa soka la kushambulia ni upuuzi, jamaa aliweka rekodi ya kumaliza na pointi nyingi England na Hispania na huwezi kufanya hilo kwa kupaki basi.
Na hiyo ndio maana timu hii itakuwa kama Chelsea ya wakati ule, iliyokuwa na vipaji vya ukweli vya Arjen Robben, Eidur Gudjohnsen na Joe Cole.

Nyuma yao kulikuwa na Claude Makelele, kiungo bora zaidi wa ulinzi kuwahi kutokea duniani na ufunguo wa mafanikio ya Chelsea kwenye miaka hiyo.
Lakini muundo mpya safari hii, utashuhudia watu wawili wakiwa na jukumu hilo, kwanza Lampard, mfungaji bora muda wote wa Chelsea, akiwa na majukumu kama Xabi Alonso ya kuanzisha mashambulizi kutoka chini.

Jamaa pia anaweza kupanda mbele mwenyewe na kuendelea kucheka na nyavu, akicheza sambamba naye atakuwa Luka Modric. Mourinho alimpeleka Real Madrid mwaka jana.
Mourinho anamuamini kiungo huyo licha ya watu Hispania kumponda. Modric ni mmoja kati ya wachezaji wawili ambao Mreno huyo atakuja nao Stamford Bridge, kutoka Santiago Bernabeu.

Mwingine siyo Cristiano Ronaldo, bali ni Raphael Varane kinda wa Kifaransa mwenye miaka 20, ambaye anatabiriwa kuja kuwa mmoja kati ya mabeki bora wa kati duniani.
Varane pia anaweza kucheza kama kiungo wa ulinzi au mfagiaji (sweeper), lakini la kwanza kwa Mourinho ni kuwa anampenda na kumuamini kinda huyo anapocheza kama beki. Madrid hawataki kumuuza, Special One hataki kuelewa hilo.

Mourinho anasema anasubiri kucheza na David Luiz, beki asiyetabirika, lakini soka la kujilipua la Mbrazil huyo litamkera Mourinho na anaweza kumfungulia milango mapema tu.
Luiz atapata nafasi, japokuwa Terry atarudisha namba yake, huyu ni mwanajeshi wa Mourinho tangu zamani na itaendelea kuwa hivyo.

Beki ya pembeni Mourinho atapata huduma nzuri kutoka kwa Ashley Cole na Cesar Azpilicueta.
Wawili hawa wako fasta kwenye kushambulia na watawapa Lampard na Modric wigo mpana zaidi wa kuanzisha mashambulizi kutoka kati kati ya uwanja.
Lakini cha muhimu zaidi ni kuwa wawili hawa wanajua kukaba.

Mwisho kabisa, kuna kipenzi kingine cha Mourinho, kipa Cech, ushujaa wake umeipa taji Chelsea msimu uliopita na kumaliza kwenye tatu bora katika ligi.
Kwa kiwango hicho na ujio wa Mourinho, mafanikio yatakuwa mengi zaidi msimu ujao.
Thibaut Courtois kipa aliye kwa mkopo Atletico Madrid, atarudishwa ilikumpa changamoto Cech katika goli la Chelsea.

Kwenye benchi Mourinho atatamani kumuona mchezaji wake wa zamani alipokuwa Inter Milan, Wesley Sneijder akisubiri kuongeza nguvu kwenye utatu mtakatifu.
Mourinho ameendelea kuwa karibu na staa huyo wa Kiholanzi, ambaye hana amani Galatasaray tangu alipotua huko kwa ada ya pauni milioni 7, Januari mwaka huu.
Demba Ba na Romelu Lukaku watakuwa wakisubiri. Ramires anaweza kucheza kama beki wa kulia, kiungo wa kulia au kiungo wa ulinzi wakati Luiz na Branislav Ivanovic watakuwa wakisubiri nje.
Mashabiki wa Chelsea wanasubiri kwa hamu kumuona Mourinho kazini.

Jeshi kamili la Mourinho
Kikosi
Kipa: Petr Cech
Beki wa kulia: Cesar Azpilicueta
Beki wa kati: Raphael Varane
Beki wa kati: John Terry
Beki wa kushoto: Ashley Cole
Kiungo wa ulinzi: Luka Modric
Kiungo wa ulinzi: Frank Lampard
Kiungo wa pembeni:Eden Hazard
Kiungo wa pembeni:Oscar
Kiungo mshambuliaji: Juan Mata
Mshambuliaji: Edinson Cavani
Mfumo: 4-2-3-1

Benchi
Courtois
Ivanovic
Luiz
Ramires
Ba
Sneijder

Lukaku

No comments:

Post a Comment