Pages

Thursday, June 6, 2013

EVRA ATAKIWA KURUDI MONACO, DZEKO CHAGUO LA MOURIHNO NA FERNANDINHO KUMTANGULIA PELLEGRINI CITY

BEKI wa Manchester United, Patrice Evra anajiandaa kutua Monaco.

Kocha ajaye wa United, David Moyes anataka kutua na beki namba tatu wa Everton, Leighton Baines, huku Evra akipata ushawishi mkubwa kutoka kwa mkewe anayemtaka warudi kwao, Ufaransa.

Evra alijiunga na United 2006 akitokea Monaco kwa pauni milioni 5.5.

Dzeko chaguo la kwanza la Mourinho

KATIKA orodha ya wachezaji Jose Mourinho anaotaka kuwasajili Chelsea majira haya ya joto, Edin Dzeko ndiye chaguo lake la kwanza.

Hata hivyo, Manchester City haitaki kumuuza mshambuliaji huyo kwa washindani wao wa ubingwa wa England, lakini Mourinho anaamini atatumia mbinu mbadala kuweza kumpata.

City kama ilivyo kwa Chelsea, zote zinamhitaji Mshambuliaji wa Napoli, Edinson Cavani ambaye anaelezwa kuwa na thamani ya pauni milioni 60, hivyo Mourinho anaamini kama akilegeza uzi katika mbio hizo, basi anaweza kumnasa Dzeko.

Benteke kupishana na Defoe Spurs

Tottenham inataka kumtoa Jermain Defoe kwa Aston Villa sambamba na fedha, ili kuweza kummiliki Mshambuliaji wao, Christian Benteke.

Klabu hiyo ya Kaskazini mwa London inataka kufanya usajili huo wakushtukiza kwa kumtoa kipenzi cha mashabiki wa England, Defoe.

Hivi karibuni, Villa ilikataa kutoa nafasi ya kumsajili Defoe, 30, na badala yake ikaelekeza nguvu zake katika kumpa Benteke mkataba wa muda mrefu zaidi.


Fernandinho kumtangulia Pellegrini City

SIKU ambayo Seville imetangaza dili la kumuuza winga wao, Jesus Navas kwa pauni milioni 22 kwa Man City, Klabu hiyo ya England imethibitisha dili lingine la kumsajili Kiungo wa Shakhtar Donetsk, Fernandinho, 28.

Klabu hiyo ipo katika mazungumzo ya kununua mkataba wake ambao unaaminika kuwa na thamani ya pauni milioni 15 na hivyo kuwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa kabla hata Kocha mpya, Manuel Pellegrini hajatua Etihad.


Mourinho amtaka Matic arudi Chelsea

KIUNGO wa Benfica, Nemanja Matic ameendelea kuhusishwa na kurudi Chelsea.

Taarifa zimeeleza kuwa, Jose Mourinho pia anataka kutua Chelsea na beki wa kushoto wa Real Madrid, Fabio Coentrao, ambaye anaamini kwamba atawekwa sokoni.

Julai 2011, Real ililipa kiasi cha pauni milioni 25 kwa beki huyo mwenye miaka 25, lakini inaaminika kuwa dau lake sasa ni pauni milioni 18.


Arsenal yatangaza dau la Sagna


Arsenal inahitaji pauni milioni tano tu, ili kumwachia beki wake, Bacary Sagna.

Gazeti la "The London Evening Standard", limeeleza kuwa Kocha Arsene Wenger anataka suala la Sagna kuamuliwa haraka na kwamba atahitaji pauni milioni tano tu.

Arsenal imeendelea kumfukuzia Beki wa Borussia Dortmund, Lukasz Piszczek ili arithi mikoba ya Sagna, lakini anaelezwa bado amebakiza miaka mitatu katika mkataba wake na kwamba huenda zikahitajika pauni milioni 10 ili kuipata huduma yake.



Man Utd yamtega Strootman 

KLABU ya Manchester United imeelekeza macho yake yote kwa Kiungo wa PSV Eindhoven, Kevin Strootman.

 Gazeti la "The Daily Mail", limeeleza kuwa United inataka kummiliki kiungo huyo wa PSV Eindhoven anayeelezwa kuwa na thamani ya pauni milioni 25.

Kiungo huyo wa Kimataifa wa Uholanzi, pia amekuwa katika rada za Everton msimu huu.



No comments:

Post a Comment