Pages

Thursday, June 6, 2013

BRADLEY SMITH RUKSA MBIO ZA CATALUNYA, HUKU NYOTA WA NORWICH CITY LEON Mc KENZIE AKIGEUKIA MASUMBWI

 MADRID, Hispania

DEREVA mahiri wa mbio za pikipiki, Bradley Smith, ameruhusiwa kushiriki  mbio za Catalunya MotoGP, ambazo zitaanza kutimua vumbi baadaye mwezi huu, baada ya kupona majeraha yaliyokuwa yakimkabili.

Awali Smith, 22, alikuwa amezuiwa kushiriki mbio hizo baada ya kutenguka mguu na kidole na kupata michubuko juu ya jicho kwenye ajali aliyoipata Jumapili wakati wa michuano ya Italia Grand Prix, lakini akamaliza kwa kushika nafasi ya tisa.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, nyota huyo aliruhusiwa juzi, baada ya kutembelewa na  madaktari mjini San Marino.

“Habari nzuri ni kwamba nitakuwa fiti kuendesha kwenye mashindano mengine ya  Barcelona.
"Habari mbaya za kuvunjika mfupa wa mguuni na kutenguka kidole kwenye mguu wangu wa kushoto nitakuwa nimeondokana nazo kabla ya mashindano hayo,” alisema dereva huyo.

Hata hivyo, madaktari hawakuweza kumfanyia upasuaji wa ngozi ya kidole kutokana na kuwa ilikuwa imeharibika vibaya, lakini wanasema kuwa vyote vitakuwa vimepona kabla ya kuanza mbio hizo.


Nyota wa zamani Norwich City ageukia masumbwi

LONDON, England
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Timu ya   Norwich City, Leon McKenzie, anajiandaa kujitosa kwenye ngumi za kulipwa baadaye mwezi huu, akiwa na umri wa miaka 35.
McKenzie, ambaye aliweza kufunga mabao  115  katika mechi 405 alizochezea klabu nane tofauti kabla ya kustaafu mchezo huo mwaka  2011, mjomba wake  aitwaye  Duke ni bingwa mara tano wa dunia wakati baba yake,  Clinton  amewahi kutwaa ubingwa wa Uingereza na Ulaya.
"Ningependa kujiunga na mchezo huo na wala sitahitaji kuachana nao tena," mwanasoka huyo wa zamani aliiambia BBC East Sport. "Nina umri wa miaka 35, hivyo sitaweza kucheza kwa muda mrefu, lakini nina imani nitafikia mafanikio yoyote," aliongeza bondia huyo.

Alisema kuwa kwa  miezi kadhaa amekuwa akijifua kambini kwake  na kwamba amekuwa akiamka saa 11 kukimbia na amekuwa akifanya kile anachoweza kukifanya.


McKenzie, ambaye  alianzia kibarua chake katika timu ya  Crystal Palace, alicheza msimu wa Ligi Kuu akiwa na timu ya Norwich  msimu wa 2004-05 na ndiye aliyefunga mabao  mawili yaliyoipatia ushindi timu yake wa 2-0 dhidi ya Manchester United, kabla ya kuhamia katika  timu za  Fulham, Peterborough, Charlton, Coventry, Northampton na Kettering.

No comments:

Post a Comment