Pages

Sunday, May 19, 2013

YANGA NI ZAIDI YA UBINGWA



NI zaidi ya ubingwa, ni zaidi ya sherehe; ndicho unachoweza kusema baada ya Yanga kunogesha 'pati lao' la
kutwaa taji la 24 la Ligi Kuu Bara kufunga msimu na ushindi safi katika mchezo dhidi ya mahasimu wao uliofanyika jana kwenye Uwanja wa wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga, ambayo tayari ilishatangazwa kuwa mabingwa wa msimu huu wa Ligi Kuu, ilinogesha sherehe zake za kukabidhiwa taji hilo katika mchezo wa mwisho ambao waliweza kuibamiza Simba mabao 2-0 na kuweza kutimiza furaha yao ya kunyakua ubingwa huku wakiwanyuka mahasimu wao hao.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefunga msimu huu kwa kukusanya pointi 60, pointi nane zaidi ya Azam FC kwenye nafasi ya pili na pointi 15 zaidi ya mahasimu wao hao, Simba, ambao wamemaliza ligi kwenye nafasi ya tatu.

Mchezo huo uliovutia mashabiki wengi kutoka pande zote za nchi hiyo na kuchezeshwa na mwamuzi, Martin Saanya kutoka Morogoro, Yanga iliweza kufungua akaunti yake ya mabao mapema katika dakika ya tano tu kupitia Didier Kavumbangu, aliyefunga kwa kichwa baada ya kona iliyopigwa kwenye lango la Simba lililokuwa likilindwa na Juma Kaseja.
Bao hilo liliweza kudumu hadi mapumziko, ambapo vijana hao wa Mholanzi, Ernie Brandts waliokuwa wameweka kambi yao visiwani Pemba walikwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilipata nafasi ya kusawazisha katika kipindi hicho cha kwanza baada ya kupata penalti, lakini ilishindwa kutumia faida hiyo.
Ilikuwa katika dakika 27, ambapo winga hatari Mrisho Ngassa alichezewa madhambi na kuangushwa ndani ya boksi na beki Nadir Haroub 'Cannavaro' na kumfanya mwamuzi Saanya kuamuru ipigwe penalti, ambapo Mussa Mudde alishindwa kutumia faida hiyo kwa kumpiga mkwaju huo mikononi mwa kipa wa Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuudaka.
Kukosa penalti hiyo kuliishusha ari kidogo Simba, licha ya kushuhudia wakipoteza nafasi kadha za kufunga, huku ukuta wa Yanga uliokuwa ukiongozwa na Cannavaro na Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na David Luhende kufanya kazi kubwa ya kumlinda kipa wao, Barthez.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga waliendelea kulisakama goli la wapinzani wao Simba na hatimaye kufanikiwa kufunga bao la pili lililowahakikishia ushindi wao katika mchezo huo.

MABAO
Didier Kavumbangu, aliyeandikia bao la kwanza Yanga katika mchezo huo, aliweza kutikisa nyavu baada ya kutumia udhaifu wa mabeki wa Simba, ambao walimwacha peke yake wakati aliporuka kichwa kwa kujizungusha mwili na kumtesa kipa Kaseja.
Shambulizi hilo lililovaa bao lilikuja baada ya kona iliyochongwa kutoka wingi ya kulia na kiungo, Haruna Niyonzima, ambapo ni kushoto kwa upande wa Kaseja, ilionekana kama haina madhara, lakini kitendo cha mabeki wa Simba kumwaacha huru Kavumbagu kiliwagharimu na hatimaye kutikisa bao hilo lililowainua mashabiki wa timu tangu dakika ya tano ya mchezo.
Kona hiyo iliyokana na shambulizi lililopangwa na Simon Msuva kwenye wingi ya kulia, ulimsababisha beki Haruna Shamte kuutoa mpira nje.
Wakifungwa bao hilo baada ya tukio la mipira ya adhabu, jambo hilo lilizidi kuwaonyesha Simba kuwa ni wadhaifu wa mipira ya aina hiyo baada ya kuruhusu bao jingine katika kipindi cha pili baada ya mpira wa kurushwa kumkukuta kweupe Hamis Kiiza na kuukwaamisha nyavuni kwa staili ya aina yake.
Twite alirusha mpira kutoka upande wa kulia, karibu kidogo na kibendera cha kona, mpira ambao kabla ya kumfikia Kiiza 'Diego', ulionekana kumbabatiza mchezaji wa Simba kabla ya mfungaji kutumia tena faida ya kujisahau kwa mabeki wa Wekundu hao wa Msimbazi kuusukuma mpira nyavuni na kuifanya timu yake kuongoza kwa mabao 2-0, ushindi ambao ulidumu hadi filimbi ya mwisho.
  
WASHAMBULIAJI
Kama kuna kocha ambaye atajivunia kikosi chake au washambuliaji wake katika mchezo huo basi ni Brandts wa Yanga, ambao ushindi wao wa mabao 2-0, shukrani kwa kazi nzuri za Kavumbagu na Kiiza.
Kwa upande wa Simba, Ngassa alipoteza nafasi moja nzuri, ambapo shuti lake lilipaa pembeni ya goli, huku Felix Sunzu naye akishindwa kutumia nafasi kadha alizopata baada ya kuingia akitokea benchi.

MABEKI
Ukitazama aina ya mabao ambayo Simba ilifungwa na kusababisha kupoteza mchezo huo wa jana ilitokana na kukosekana kwa umakini kwenye safu ya ulinzi, tofauti na wenzao Yanga - ambao ilikuwa imara zaidi kwenye safu yake ya ulinzi na kuhakikisha inazima mashambulizi yote yaliyoelezwa kwa goli lao.
Simba wao mabeki wao walitoa nafasi kwa washambuliaji wa Yanga kuwa huru, jambo ambalo walilitumia kuwaadhibu kwa kuwafunga mabao hayo mawili.
Kwa upande wa Yanga, safu yake ya ulinzi ilichokuwa ikifanya ni kuhakikisha mipira yote inayomfikia kipa wao, Barthez ni ile ambayo haina madhara sana.

MABADILIKO
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig kwa upande wake alifanya mabadiliko ya wachezaji watatu, ambapo aliwaigiza Sunzu, Jonas Mkude na Ramadhan Singano 'Messi' kuchukua nafasi za akina Abdallah Seseme, Amri Kiemba na Haruna Chanongo, mabadiliko ambayo yalionekana kubadilisha kasi ya mchezo kwa Simba na kuwapa presha mabeki wa Yanga katika dakika 10 za mwisho.
Messi, alionekana kuwa tishio zaidi kwa mabeki hao wa Yanga na kumsumbua Luhende mara kadha, licha ya beki huyo wa kushoto kucheza soka la aina yake katika mechi hiyo ya watani kwa jana.
Lakini, ilionekana kama amechelewa sana kocha Liewig kufanya mabadiliko hayo, kwasababu licha ya purukushani kadha kwenye goli la Yanga, mabingwa hao waliweza kuhimili vishindo na kuweza kutimiza ahadi yao ya kuifunga Simba.
Brandts yeye alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili ambapo aliwatoa Twite na Kiiza na nafasi zao kuingia, Nizar Khalfan na Juma Abdul, mabadiliko ambayo nusura yazaye bao la tatu baada ya shuti laki la mpira wa adhabu lililopigwa na Nizar kugonga mwamba kabla ya kumjeruhu Kaseja kichwani na kumfanya ahitaji huduma ya kidaktari kwa dakika kadha.
Nizar alifyatuka shuti lake nje ya eneo la 18, ambapo shuti hilo Kaseja aliliguswa kidogo kabla ya kwenda kugonga mwamba na kurudi uwanjani kupiga kichwani kipa huyo na kupata maumivu.

VITUKO
Kituko kikubwa ambacho kilionekana kuwavutia wengi ni pale shabiki wa Yanga, aliyekuwa amejipaka masizi na kuvaa nguo zenye rangi ya jezi za klabu hiyo kwenda kulishika kombe lililokuwa limewekwa pembeni ikisubiriwa kukabidhiwa kwa mabingwa.
Lakini, kama kituko hicho hakitoshi, baada ya filimbi ya mwisho na tukio la kugawa medali kumalizika na Yanga wakiwa wamekabidhiwa taji lao hilo, kundi la mashabiki wa Yanga walionekana wakimbeba juu juu fowadi wa Simba, Ngassa - huku wakiwa wamemvisha jezi yenye rangi ya kijani na nyano.
Wakati hilo likifanyika, kwenye jukwaa la mashabiki hao wa Yanga, kulikuwa na bango lililoandikwa 'Ngassa mwana mpotevu karibu nyumbani', tukio ambalo lilikwenda sambamba na mashabiki hao waliokuwa wamembeba juu juu mkali huyo wa kimataifa wa Tanzania.

MWAMUZI
Mara kadha kumekuwa na malalamiko kwa waamuzi zinapokuja kuchezesha mechi kama hizi za watani, lakini kwa refa wa mchezo huo wa jana, Saanya, haikuwa siku ngumu sana kwake kwani alionekana kumiliki vizuri mchezo kabla ya kutokea kwa tukio la kujeruhiwa jichoni na kutoka damu wakati alipokwenda kujaribu kuzuia ugomvi baina ya Kavumbangu na Nassor Masoud ‘Chollo’  na hivyo alianguka na kutibiwa kwa dakika kadha hadi alipoinuka kuendelea na mchezo kwa sekunde chache na kupiga filimbi ya mwisho kuhitimisha dakika 90.

VIKOSI  
Simba SC: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna Shamte, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, William Lucian ‘Gallas’, Mrisho Ngassa, Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme/Ranmadhani Singano ‘Messi’, Amri Kiemba/Jonas Mkude na Haruna Chanongo/Felix Sunzu.
Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan,  Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza/Niaar Khalfan.

MATOKEO MENGINE
Wakati pazia la Ligi Kuu Bara likiwa limefungwa rasmi jana, viwanja kadha vingine vilishuhudia mechi kali kabisa, ambapo JKT Oljoro walikubali kichapo cha mabao 1-0 kutoka kwa Azam, huku JKT Mgambo wakiinyuka African Lyon mabao  1-0, Toto Africans wakiishinda Ruvu Shooting 2-0, JKT Ruvu waliikamua Mtibwa Sugar 1-0 na Tanzania Prison ilinyukwa 1-0 na Kagera Sugar na Polisi Moro kuichapa Coastal Union 2-0.




No comments:

Post a Comment