Pages

Thursday, May 30, 2013

DIAMOND, NEY WA MITEGO NA MADEE KUTUMBUIZA SHINDANO LA QS DAR LIVE JUMAMOSI

ONYESHO kubwa ambalo ni uzinduzi wa Shindano la QS Queens 'Utamu Extra' linalotarajiwa kufanyika Jumamosi ya  Juni Mosi katika Ukumbi wa Dar Live, Mbagala, pia limepangwa kuwa sehemu maalum ya kuenzi mchango wa msanii Albert Mangwea, aliyefariki nchini Afrika Kusini.

Ngwea amepangwa kuletwa kesho Jumamosi kwa ajili ya maziko yake yaliyopangwa kufanyika mkoani Morogoro, huku onyesho hilo la maombolezo likihudhuliwa na wakali kibao wa muziki hapa nchini lilioandaliwa kwa muda mrefu na kilele chake kuwa Jumamosi hii.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, leo mchana, Meneja Masoko wa Kampuni ya QS Mhonda J Entertainment, Freddy Felix, alisema kuwa shindano hilo litafanyika pia katika mikoa mbalimbali kwa ajili ya kupata warembo 20 watakaoishi katika Jumba moja kwa ajili ya kupata kimwana huyo wa QS Queens.

Alisema kuwa wasanii wengi wamepangwa kupanda jukwaani kwa ajili ya kuomboleza msiba huo, akiwamo Ney wa Mitego, Wanaume Halisi, ikiongozwa na Juma Nature, MB Dog, Diamond, Inspector Haroun, Madee, H-Baba, Snura, Khadija Kopa, Solid Ground Family na wengineo, wakiwamo wasanii chipukizi, Amor na Shalviny.

“Wasichana wote wanaotaka kushiriki shindano hili ambao ni kama uzinduzi wake, watajiandikisha katika fomu maalum ukumbini hapo, ambapo baadaye watatafutwa wengine ambao wote wataishi kwa miezi miwili katika nyumba moja itakayotembelewa na watu mbalimbali.

“Huku mshindi akijishindia gari la kifahari, pia wanapokuwa katika jumba hilo kila siku mtu atalipwa kadri tutakavyokubaliana, huku tukiamini kuwa huu utakuwa ni mwanzo mzuri katika shindano hili,” alisema Felix.

Kwa mujibu wa Felix, shindano hili kabla ya kupatikana warembo hao litatembelea mikoa kadhaa ya Tanzania Bara, kama vile Mwanza, Tanga, Morogoro, Mbeya, Iringa na kwingineko kwa ajili ya kutafuta msichana mmoja wa kuingia katika kinyang’anyiro hicho.

Aidha QS ilitangaza kuwa mabinti wanaotakiwa kushiriki katika shindano hilo ni wale wenye vipaji maalum na uwezo wowote wa kupambanua mambo, huku kigezo cha elimu kikiwekwa pembeni.

Shindano hilo pia litaonyeshwa katika vituo vya Channel Ten, DTV, Clouds, ambapo huko kote wadau na wapenzi wa mambo ya urembo na burudani watapata fursa ya kuwapigia kura washiriki kabla ya siku ya kilele chake kitakachofanyika baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment