Pages

Friday, May 31, 2013

CESC FABREGAS: Picha linaanza upyaaa!!!!!

NI miaka miwili tu imepita tangu Cesc Fabregas (26), alipoondoka London na kurudi nyumbani Barcelona, kwenye uhamisho ambao ulionekana kama hauwezi kukamilika.
Kwa wali ambao wameanza kupenda soka juzi, Fabregas aliondoka Barcelona na kutua Arsenal wakati wa kiangazi mwaka 2003 akiwa na miaka 16, kabla ya kurudi nyumbani msimu wa 2011-12.

Arsenal na Arsene Wenger wanachukulia kumuuza Fabregas kwenda Barcelona kama biashara tamu yenye chungu ndani yake. Wenger, Klabu na Mashabiki walimshuhudia Kinda wa miaka 16 waliyemnunua kwa euro milioni 3, akiwa nahodha wa timu hiyo katika umri wa miaka 24.
Hatimaye walimuuza Barcelona kwa ada ya euro milioni 34, baada ya vuta nikuvute kwa misimu mitatu ya usajili.

Mashabiki wengi wa Arsenal walisahau juu ya uhamisho wa Fabregas kwenda Barca. Wanasema kuwa kilikuwa kipindi cha kipekee, Cesc alikuwa akirudi nyumbani kuungana na wachezaji wenzake aliocheza nao utotoni, kina Gerard Pique, Lionel Messi na wengine wengi.

 Pia alikuwa akiungana na shujaa wake alipokuwa mtoto Pep Guardiola, Guardiola alikuwa ametengeneza bonge la timu, haikuwa rahisi kwa mashabiki wa Arsenal kukubaliana na uhamisho huo lakini ukweli ni kuwa Fabrigas alipata nafasi ambayo ilikuwa ngumu kuikataa.

Maisha yaliendelea London Kaskazini, japokuwa kuziba nafasi ya Fabrigas ilikuwa ngumu, Santi Cazorla ameleta kitu fulani cha Kihispaniola kwenye kiungo cha Arsenal.
Baadhi ya mashabiki wa Arsenal bado wanafuatilia maendeleo ya Fabregas, akiwa Barca. Vyombo vya habari vimekuwa vikiifuatilia sana Barcelona na ukweli kwamba mchezaji wa zamani wa Ligi Kuu England hana furaha kwenye moja ya timu bora duniani unazua maswali: Je, Fabregas yuko njiani kusepa?

Watu wanaanza kukumbuka mengi sana, matumaini, kuumizwa, kujiamini na hofu. Je, ni kweli Fabregas ataondoka Barcelona? Ni kweli Cesc ni moja kati ya viungo bora duniani. Hakuna mwenye kubisha juu ya hilo. Bahati mbaya kwake kwa sasa kuna Xavi Hernandez na Andres Iniesta.

Ujio wa Fabregas, Barcelona ulimaanisha kuwa mabadiliko kwenye kikosi cha timu hiyo, yaani Xavi alitakiwa kumpa kijiti Fabregas, lakini cha kushangaza ndio kwanza kiwango cha Xavi kinazidi kupanda na hii imemnyima nafasi Cesc ya kung’ara.
Inawezekana Fabregas akawa anafikiria kwamba, anatakiwa kusubiri na kufanya mazoezi mengi basi na yeye wakati wake utafika. Mpango huo ulikuwa mzuri mpaka wiki hii, Barca walipotangaza kumsajili Neymar, usajili huu umeharibu dili lake.

Mashabiki wa Arsenal wanashangilia! Hii inatokana na taarifa kwamba, kuna kipengele ambacho kipo kwenye mkataba wa Fabregas alipohamia Barca, ambacho kinasema kwamba The Gunners wapewe nafasi ya kwanza kama mchezaji huyo atataka kurudi England.
Wenger anaamini ipo siku Fabregas atarudi Emirates, kwa sababu mchezaji huyo anaipenda Arsenal kutoka moyoni mwake.

Swali je, kweli anaweza kurudi kwenye timu ambayo haijatwaa taji lolote kwa miaka 8? Robin Van Persie alikuwa nahodha wa Arsenal mpaka alipoamua kuhamia Manchester United alipopata taji.
Uamuzi wa RVP kuitema Arsenal na kutua Man United, ulitoa ujumbe tosha kwamba alikuwa akitaka makombe na kweli alishinda taji miezi 10, baada ya kuitema Arsenal. Kiukweli wachezaji kibao wameshinda ubingwa tangu walipohama Arsenal. Samir Nasri, Cesc Fabregas, Ashley Cole, Kolo Toure na Robin Van Persie ni baadhi ya wachezaji waliobeba taji baada ya kuondoka Emirates.

Wiki hii Fabregas amehusishwa na Manchester United. David Moyes anataka kufikisha ujumbe kwa mashabiki wa Man United kwa kufanya usajili mkubwa na njia pekee ya kufanya hivyo ni kwa kumleta nahodha wa zamani wa Arsenal.
Fabregas ameshatwaa taji la Euro mara mbili, Kombe la Dunia mara moja, La Liga mara moja na Kombe la FA akiwa na Arsenal mwaka 2005. Kariba yake ya kupenda ushindani haiwezi kumruhusu kuendelea kusugua benchi Barcelona, kariba yake ya ushindani itampeleka sehemu atakayopata mataji zaidi.

Kuna ukweli kuhusu nia ya Moyes kumtaka Fabregas. Kocha huyo mpya wa Man United anahitaji kuimarisha sehemu ambazo zitaathiriwa na kuondoka kwa Paul Scholes.
Anderson naye anaonekana yuko njiani, Nani pia, mchanganyiko wa vijana na wazoefu huku Tom Cleverley na Michael Carrick wakiwa vizuri, itakuwa jambo zuri kwake kuongeza kiungo mwenye uwezo kama wa Fabregas usajili huu utaipeleka Man United levo nyingine.
Haijalishi Fabregas anaipenda Man United ama la, kitu kimoja kiko wazi mashabiki wa Arsenal wanatakiwa kusubiri sakata jingine ambalo litamshuhudia nahodha wao wa zamani akitua kwenye klabu nyingine.

No comments:

Post a Comment