Pages

Wednesday, April 24, 2013

YANGA KWENDA NJE KUWEKA KAMBI KWA AJILI YA KAGAME


Kwa mara nyingine wachezaji wa Yanga wataenda kuweka kambi nje ya nchi kwa ajili ya maandalizi ya kutetea taji lao la mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yatakayofanyika mwezi Juni mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Hata hivyo, bado kocha wa timu hiyo, Mholanzi Ernie Brandts hakuwa tayari kusema ni nchi gani kikosi hicho kitakwenda kujifua kwa ajili ya michuano hiyo ya kila mwaka. 
Brandts  amesema kuwa kambi ya nje ya nchi husaidia kuwaimarisha wachezaji kimwili, kiakili na kuwaweka tayari kukabiliana na ushindani. 
Aliongeza kuwa wachezaji wanapokuwa nje ya nchi wanakuwa na wakati mzuri wa kufuatilia mafunzo na kuyafanyia kazi wanaporudi nchini. 

Alisema pia anafurahi kuona yuko katika wakati mzuri wa kuweza kutwaa taji la kwanza la ligi kuu akiwa na Yanga na la 23 kwa ujumla kwa klabu hiyo na anataka kuona pia wanatetea vyema ubingwa wao wa Kombe la Kagame. 
Vinara wa ligi kuu ya bara, Yanga, wanahitaji pointi moja tu kutwaa ubingwa na tayari wamejihakikishia moja ya nafasi mbili pekee za kushiriki michuano ya klabu barani Afrika.

No comments:

Post a Comment