Pages

Wednesday, April 3, 2013

WAZIRI WA UCHUKUZI MWAKYEMBE MGENI RASMI BONANZA LA VYOMBO VYA HABARI.



WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye bonanza la vyombo vya habari linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Bonanza hilo litafanyika  Jumamosi wiki hii viwanja vya Sigara, Chang’ombe, Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa moja usiku likidhaminiwa na na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).

Pamoja na mambo mengine, Waziri Mwakyembe atakabidhi zawadi za vikombe na medali kwa washindi mbalimbali watakaoibuka siku hiyo, pia atapata fursa ya kuzungumza na washiriki wa bonanza hilo.

Lengo la bonanza ni kuwaweka pamoja waandishi wote wa habari bila kujali ni wa siasa, michezo, uchumi, afya na mambo mengine, ili kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja na huwa linafanyika mara moja kwa mwaka, likiandaliwa na TASWA.

Bonanza hilo ambalo litahusisha wadau 1,500 kutoka vyombo mbalimbali vya habari litaambatana na michezo mbalimbali itakayohusisha vyombo vyote vitakavyoshiriki na pia kutakuwa na burudani ya muziki.

Tunataka bonanza la mwaka huu liwe la aina yake kuanzia mgeni rasmi, burudani, michezo na mambo mengine yawe ya kuvutia, ambapo Alhamisi Aprili 4,2013 saa tano asubuhi kutakuwa na mkutano na wanahabari mgahawa wa City Sports Lounge, Posta Dar es Salaam ambao ni maalum kutangaza makundi yatakayotumbuiza kwenye Media Day na tunatarajia makundi hayo nayo yatakuwepo kwenye mkutano huo.

Tunaomba vyombo vya habari ambavyo havijathibitisha ushiriki wao kwa njia ya maandishi vifanye hivyo kama vilivyoagizwa kwenye barua zao za mialiko, vinginevyo ushiriki wao hautathaminika.

Bonanza litaanza saa tatu asubuhi, ambapo baadhi ya michezo itakayoshindaniwa ni soka ya ufukweni, netiboli, wavu, mbio za magunia, mbio meta 100, kuruka kichura, kuvuta kamba, kucheza muziki na kuimba.
Nawasilisha.

No comments:

Post a Comment