Pages

Sunday, April 28, 2013

SUNZU: LEO NAIUA POLISI KISHA NAMALIZIA KWA YANGA



BAADA ya kupigishwa mazoezi maalumu kwa ajili ya maandalizi ya kuwavaa Yanga, mshambuliaji wa Simba, Mzambia Felix Sunzu, sasa ataanza kuonyesha makali hayo mapya katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Morogoro, utakaofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ligi hiyo, ambayo tayari Yanga imeshanyakua ubingwa, itaendelea kwa Simba wakijaribu kusaka ushindi utakaowawezesha kumaliza katika nafasi za juu baada ya mambo kwenda kombo msimu huu.
Na sasa kabla ya kuwakabili Yanga, Sunzu aliyekuwa akifanyishwa mazoezi maalumu kama mshambuliaji anayeandaliwa kuwamaliza mahasimu wao hao katika mchezo wa mwisho wa ligi hiyo, sasa anatazamiwa kufanya kile alichojifunza hii leo kwenye mechi hiyo dhidi ya Polisi Moro ili kutuma meseji kwa mahasimu wao hao.

Wakati Simba ikicheza na Polisi hii leo, lakini presha kubwa ipo kwenye mechi yao dhidi ya Yanga na kama Sunzu na wenzake waliokuwa wakifanya mazoezi maalumu, ambao ni Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude na Ramadhan Singano 'Messi', sasa fowadi huyo anasubiri kuanza kukionyesha hii leo ili kuona kama jaribio lao wanalolilenga limefanikiwa.

Simba inahitaji kuweka heshima katika mchezo wake huo dhidi ya Yanga, ambapo ikipanga kurejea kumbukumbu ya ushindi wa mechi ya mwisho ya msimu uliopita, ambapo Wekundu hao wa Msimbazi waliiangusha dozi ya nguvu kwa mahasimu wao kwa kuwachapa mabao 5-0.

Katika mchezo wa duru la kwanza uliozikutanisha timu hizo, matokeo yalikuwa bao 1-1, ambapo Amri Kiembo alifunga bao la kuongoza kwa Simba, kabla ya Said Bahanunzi kusawazisha kwa mkwaju wa penalti.

Hadi sasa Simba inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi ikiwa imekusanyia pointi 36, pointi nne nyuma ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya tatu na pointi 12 nyuma ya Azam, lakini Simba ikiwa na mechi mbili zaidi mkononi.

Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig, alizungumzia mchezo wa leo na kusema: “Bado tuna nafasi ya kushinda licha ya kupoteza taji mzimu huu, ni lazima tufanye kila njia kuweza kupata nafasi katika tatu bora.”

No comments:

Post a Comment