Pages

Sunday, April 28, 2013

SIMBA YALINDA HESHIMA TAIFA BAADA YA KUIFUNGA POLISI MORO 2-1

Mshambuliaji wa Simba Haruna Chanongo akiwa na mpira huku mchezaji wa Polisi Moro Nahoda Bakari akiangalia jinsi ya kumnyang'anya bila kuleta madhara wakati wa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Uwanja wa Taifa leo

Mshambuliaji wa Simba Felix Sunzu akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Polisi Moro Nahoda Bakari



Kiungo mshambuliaji wa Simba Amri Kiemba akiwa na mpira


Mshambuliaji wa Simba Felix Sunzu akikimbia na mpira huku mabeki wa Polisi Moro wakimkimbiza

Kikosi cha Simba

Kikosi Moro
BAO la ushindi la winga wa Simba, Mrisho Ngassa lilitosha kwa timu yake kuibuka na pointi tatu, baada ya kuifunga Polisi Morogoro mabao 2-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiwezesha timu hiyo kufikisha pointi 39, huku ikiendelea kubaki katika nafasi ya nne na Yanga ikiwa tayari imechukua ubingwa wa ligi hiyo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Mwamuzi,  Dominic Nyamisana kutoka Dodoma, Polisi ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 10 kupitia kwa Bantu Admin aliyefunga kwa shuti la mbali, ambalo lilikwenda moja kwa moja nyavuni.

Admin aliweza kufunga bao hilo baada ya kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Mokil Lambo, ambaye kabla ya kutoa pasi alipokea mpira ulioanzia kwa Basil Abdul.
Katika dakika ya 15, Ramadhan Singano ‘Messi’ wa Simba alishindwa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na Haruna Chanongo, baada ya shuti lake kuokolewa na beki wa Polisi, Nahoda Bakari.

Simba ilipoteza nafasi nyingine katika dakika ya 19, baada ya Chanongo kushindwa kufunga  aliyepaisha juu shuti lake baada ya kupokea pasi kutoka kwa winga wa timu hiyo, Mrisho Ngassa.
Katika dakika ya 27, mvua kubwa ilinyesha katika uwanja huo na kusababisha utelezi uwanjani.

Dakika ya 30, Simba waliweza kugongeana vizuri, lakini washambuliaji wao walikosa umakini, ambapo Chanongo alishindwa kumalizia pasi ya mwisho ya Amri Kiemba akiwa ndani ya eneo la hatari.
Katika dakika ya 34, Simba ilifanikisha kusawazisha bao kupitia kwa Chanongo, baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Kiemba aliyefunga kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Polisi Kondo Salum.

Kabla ya bao hilo katika dakika ya 32 Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alimnyanyua kwenye benchi mshambuliaji wa timu hiyo, Felix Sunzu kwa lengo la kutaka kuchukua nafasi ya Abdalah Seseme, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Patrick Liewig alizuia mabadiliko hayo.

Simba ilipata bao la pili katika dakika ya 47, kupitia kwa Ngassa baada kuunganisha krosi nzuri ya beki wa timu hiyo, Nassoro Masoud ‘Chollo’ aliyepanda mbele kusaidia mashambulizi. 

Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Chollo’/ Haruna Shamte, Miraji Adam, Shomari Kapombe, Mussa Mudde, Ramadhan Singano ‘Messi’, Abdallah Seseme/ Felix Sunzu, Haruna Chanongo/ Edward Christopher, William Lucian, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.

Polisi Morogoro: Kondo Salum, Rogers Gabriel, John Bosco, Abdallah Mfumo, Chacha Marwa, Nahoda Bakari, Bantu Admin, Mzamil Yasin/Ally Shomary, Mokil Lambo/ Salum Machaku, Basil Abdul/ Keneth Masumbuko na Nicholas  Kabipe.

No comments:

Post a Comment