Pages
▼
Tuesday, April 23, 2013
NJIA ILIYOPITA MAN UNITED HADI KUTWAA TAJI LA 20 UINGEREZA
LONDON, England
MANCHESTER United ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu, ikiwa ni taji lake la 20, huku ikifanya hivyo kukiwa kumebaki mechi nne kabla ya kumalizika kwa msimu.
Dimba linakuletea njia iliyopita Man United katika kutwaa ubingwa huo kuanzia mwanzo wa msimu hadi sasa, ambapo timu hiyo inayonolewa na Mskochi Sir Alex Ferguson, imetumia miezi tisa tu kuubeba ubingwa huo kwa msimu wa 2012-13.
AGOSTI
Man United ilianza kampeni yake ya kuurudisha ubingwa huo uliokuwa umenyakuliwa na Manchester City, kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Everton, saa 24 baada ya mabingwa kuanza msimu wao kwa ushindi wa 3-2 nyumbani kwa Southampton iliyokuwa imepanda daraja.
Lakini, Robin van Persie, ambaye aliichezea United kwa mara ya kwanza kwenye ligi akitokea benchi kwenye mechi hiyo ya kichapo, aliweza kukaribishwa vizuri na wachezaji wenzake katika timu hiyo wakati waliposhinda 3-2 dhidi ya Fulham, wakati huo City wakiwa wamebanwa na Liverpool na kutoka nao sare ya mabao 2-2.
SEPTEMBA
Van Persie alidhihirisha kwanini Ferguson alikubali kutumia karibu milioni 24 kuinasa saini yake kutoka Arsenal, baada ya Mdachi huyo kufunga mara mbili katika dakika tatu za mwisho kukamilisha 'hat-trick' yake katika mechi ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Southampton.
Van Persie alifanya vizuri pia katika mechi dhidi ya Liverpool, wakati mkwaju wake wa penalti katika dakika za lala salama kuwasaidia kushinda 2-1, lakini ushindi wa mechi nne mfululizo wa United ulifika kikomo mbele ya Tottenham Hotspur, ambao walishinda 3-2 kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Old Trafford tangu mwaka 1989.
Bahati nzuri kwa United, Man City nao walitoka sare na Stoke City na Arsenal kutibua mipango yao ya awali ya kutetea ubingwa huo.
OKTOBA
Kulikuwa na mvuto mkubwa wa kuitazama wakati walipoinyuka Newcastle United 3-0 kwenye Uwanja wa St James' Park na kisha ikafunga mara nne dhidi ya Stoke, kabla ya bao la dakika za jioni la Javier Hernandez, kuipa United ushindi wa 3-2 dhidi ya Chelsea iliyokuwa na wachezaji tisa uwanjani.
Matokeo hayo yaliifanya United kuwa nyuma kwa pointi moja dhidi ya vinara Chelsea na nafasi moja juu ya Man City, ambapo iliweza kupata ushindi wa mechi tatu dhidi ya Sunderland, West Bromwich Albion na Swansea City.
NOVEMBA
Van Persie alitumia dakika tatu kufunga bao katika mechi dhidi ya klabu yake ya zamani Arsenal, katika mchezo ambao walishinda 2-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford na wiki iliyofuata Hernandez alifunga mara mbili kuisaidia United kutoka nyuma na kushinda 3-2 dhidi ya Aston Villa.
Kichapo cha kushitukiza cha 1-0 kutoka kwa Norwich City, kiliibua maswali kama United itaweza kubaki kileleni, lakini Man City ilishindwa kutumia fursa hiyo baada ya kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Chelsea, katika mechi ya kwanza kabisa ya Rafael Benitez katika kibarua chake Chelsea na kuwafanya City kuendelea kuwa kwenye nafasi nzuri katika kuelekea Krismasi.
DESEMBA
Ubovu wa safu ya ulinzi ya United ulitoa zawadi ya Krismasi, lakini mabao kutoka kwa van Persie na Wayne Rooney yaliweza kuisaidia timu hiyo kushinda mechi tano kati ya sita kwenye mwezi huo.
Ushindi wa 4-3 dhidi ya Reading ulifuatiwa na wa 3-2 dhidi ya Man City, huku van Persie akizidi kuing'arisha timu hiyo ya Old Trafford.
Man City ilikumbana na wakati mgumu tena Desemba 23, wakati United walipopambana kutoka nyuma kuifunga Newcastle 4-3, wakati mabingwa watetezi wa wakati huo walinyukwa 1-0 na Sunderland na hivyo kuachwa kwa pointi saba nyuma.
JANUARI
Bao la dakika za mwisho la Clint Dempsey lilitosha kuisaidia Spurs kusawazisha na mechi hiyo kumalizika kwa sare ya 1-1 White Hart Lane na hivyo United kushindwa kushinda mechi yake ya mfululizo mwanzoni mwa Mwaka Mpya.
Ushindi wa 2-1 nyumbani dhidi ya Liverpool, ulikuwa na faida kubwa kwa United, wakati Man City walishinda mechi tatu kati ya nne, ikiwamo ushindi wa 2-0 dhidi ya Arsenal, lakini bado waliendelea kuwa nyuma kwa pointi.
Kutokana na Chelsea tayari kuwa nyuma kwa pointi 13, hivyo mbio za ubingwa zilikuwa za timu mbili pekee.
FEBRUARI
United walizichapa Fulham, Everton na Queens Park Rangers bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa na hivyo kuzidi kuwachanganya mahasimu wao Man City.
Man City inayonolewa na Roberto Mancini, ilibanwa na kutoka sare ya bao 2-2 dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Etihad Stadium na kisha kuduwazwa kwa kipigo cha 3-1 dhidi ya Southampton.
Man City ilizinduka na kuifunga Chelsea 2-0, lakini wakati huo pengo la pointi liliongezeka na kufikia 13.
MACHI
Kiungo Mjapan, Shinji Kagawa alifunga 'hat-trick' katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Norwich na kufuatiwa na ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Reading na Sunderland ulizidi kuwapa pointi muhimu na hivyo kuzidi kuiacha Man City katika mbio hizo.
Man City ilipoteza njaa ya kusaka taji hasa baada ya kichapo cha 2-0 kutoka kwa Everton na jambo hilo liliifanya United kuwa mbele kwa pointi 15 na hivyo kuwa na uhakika wa asilimia kubwa ya kutwaa ubingwa huo.
APRILI
Man City ililinda heshima yake baada ya kushinda 2-1 Old Trafford, wakati Sergio Aguero alipofunga bao maridadi kabisa la juhudi binafsi katika dakika 78 baada ya James Milner kufunga la utangulizi, kabla ya Vincent Kompany kujifunga na kuisawazishia United.
Hata hivyo, United ilikuwa tayari imeweka mkono mmoja kwenye taji baada ya sare yao ya 2-2 dhidi ya West Ham United, huku Man City wakikumbana na kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Tottenham na kumfanya United kuhitaji pointi tatu tu kutangaza ubingwa, kitu ambacho walikifanya kwa kuichapa Aston Villa 3-0 juzi usiku, shukrani kwa mabao matatu ya fowadi wa Uholanzi, Robin van Persie.
No comments:
Post a Comment