Pages

Tuesday, April 23, 2013

HAYA YANATOSHA LIVERPOOL KUACHANA NA LUIS SUAREZ

LUIS SUAREZ (Liverpool)

LIVERPOOL, England
LUIS Suarez, hakuna shaka juu ya uwezo wake wa kisoka ndani ya uwanja. Hakuna shaka kwamba, ni silaha inayotegemewa na Liverpool katika miaka ya hivi karibuni. Lakini, tabia yake ndio inayotia shaka.
Suarez anaiweka klabu hiyo katika taswira mbaya, anachafua hadhi ya klabu, ambayo ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na mabingwa mara 18 wa England.

Mwaka 2010, katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini, taifa lake la Uruguay, lilimwona kuwa shujaa, baada ya kuiokoa timu yake kwa kudaka makusudi mpira uliokuwa unakwenda kwenye nyavu katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo dhidi ya Ghana.
Baada ya tukio hilo, Suarez alitolewa kwa kadi nyekundu, lakini ilipopigwa penalti, Asamoah Gyan, alikosa na hivyo Uruguay kuweza kushinda vita hiyo kwa kutinga robo fainali ya mikikimikiki hiyo mikubwa kabisa katika mchezo huo wa soka.

Aliporudi kwenye klabu yake ya Liverpool, akafanya tukio jingine ambalo lilimlazimu kuwa nje ya uwanja kwa mechi nane. Jambo hilo liliigharimu klabu yake, kwasababu ilimkosa katika mechi muhimu.
Lakini, hilo halikuwa na madhara makubwa kwa hadhi ya klabu, kwasababu ilionekana ni timu inayofuga wachezaji wenye ubaguzi. Kilichomponza Suarez hapo ni kutumia lugha ambayo ilionekana kama ubaguzi wa beki wa mahasimu wao wa jadi, Manchester United, Mfaransa Patrice Evra.

Liverpool ilichukua suala la ubaguzi kama kitu kilichowachefua na hivyo kumtaka mchezaji huyo abadilike, ikiwamo kuachana na mpango wake wa kugoma kumpa mkono Evra, tukio ambalo alilifanya na kujikuta akizomewa na mashabiki wa soka wasiopenda masuala kama hayo.
Na sasa Liverpool wanapaswa kunawa mikono kutokana na kilichotokea Jumapili kwenye uwanja wao wa nyumbani wa Anfield, walipomenyana na Chelsea.

Wamiliki wa klabu hiyo, Wamarekani lazima watakasirishwa na tukio lake alilofanya hivi karibuni, kwasababu litachafua sura ya klabu hiyo, hasa ukizingatia hivi karibuni walitibuliwa kwa milipuko ya mabomu katika mashindano ya mbio ndefu za Boston Marathon, iliyotokea Jumatatu iliyopita.
Jambo hilo pia litawatibua wadhamini wakuu wa klabu hiyo. Usiku wa juzi, Chama cha soka England (FA), kilisema kitatazama picha za video kutazama tukio la kung'ata la mchezaji Suarez, ambaye alimtia meno mkononi beki wa Chelsea, Branislav Ivanovic, tukio ambalo dunia nzima ililiona kama ni unyama.

Ni wazi kabisa FA haitaweza kulifumbia macho jambo hilo. Hakuna pointi dhaifu ya kudai kwamba, mwamuzi hakuona jambo na kwasababu hakuliweka kwenye ripoti yake basi mchezaji huyo aponyeke kwenye hilo.
Mara kadha, FA imekuwa ikijificha kwenye kichaka hiki, wakibainisha juu ya maelekezo ya Shirikisho la kimataifa la vyama vya soka (FIFA).
Kwenye hili, hilo lisipewe nafasi kabisa. Rais wa Fifa, Sepp Blatter, hivi karibuni masuala mengine yanahusu binafsi na hivyo uamuzi ni juu yao.

Kuonyesha kwamba wamekerwa na jambo hilo, Liverpool wamempiga faini Suarez kwa kumkata mshahara wake wa wiki nne, ambapo ni kati ya pauni 200,000 hadi 400,000, licha ya kubainisha kwamba, itaendelea kubaki na huduma ya straika huyo.
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema, kutenda kosa si kosa, ila kurudia kosa; hivyo kwa kulitazama hilo kuna kila sababu za Suarez kukumbana na adhabu kali na pengine Liverpool wafikirie mara mbili ya kuendelea kubaki na huduma ya staa huyo.

Kutokana na fowadi huyo kuwahi kufungiwa mechi saba wakati alipokuwa akiichezea Ajax kwa ajili ya kumng'ata shingoni mchezaji wa PSV, Otman Bakkal mwaka 2010, jambo hili linaonekana kutisha.
Tukio hilo lilimfanya mchezaji huyo kupachikwa jina la “The Cannibal of Amsterdam”, wakiwa na maana ya mla nyama za watu wa Amsterdam. Na tangu hapo, kila alipokwenda Suarez amekuwa akitengeneza kumbukumbu mbili kubwa, furaha na huzuni.

Uwezo wake wa kiuchezaji hauna shaka hata kidogo. Kwenye mchezo huo dhidi ya Chelsea, Suarez aliweza kufunga bao lake la 30 msimu huu, wakati aliposawazisha katika dakika 97, ikiwa ni idadi kubwa ya mabao kuwahi kufikiwa na mchezaji mmoja tangu Fernando Torres alipoondoka.
Kwa Liverpool hapa yeye ni shujaa na gwiji, lakini kwa mashabiki wengine wa soka mshambuliaji huyo, 26, anaonekana kama kituko.

Mchezaji huyo kwa sasa ameshindwa kuonyesha kuwa yupo upande gani, haendani na kokote, iwe kwenye sheria za mchezo huo katika jamii kwa ujumla. Mtu ambaye hajifunzi kutokana na makosa.
Ni wiki hii, Liverpool inakumbuka miaka 24 ya tukio la Hillsborough, ambapo kwenye mchezo huo walitumia dakika moja ya kukaa kimya, kabla ya Suarez kuibuka na tukio lake hilo la kipuuzi.
Wanasoka wamekuwa wakichukuliwa tofauti sana na kesi zao na kuwa na sheria tofauti na ilivyo kwa watu wengine, lakini sasa kwa staili hii kuna kila sababu ya wachezaji nao wangekuwa wanaadhibiwa kwa sheria zinazowabana raia wa kawaida.

Kiukweli, Liverpool haitakuwa imeingia hasara kama itakubali kumpiga bei mchezaji huyo, ili tu kulinda hadhi yao. Kuweka kibindoni
pauni 35 kwa mauzo ya mchezaji huyo, ambaye klabu za Bayern Munich, PSG na Barcelona zinaonyesha kumtaka haitakuwa hasara kwao na hapo Liverpool itakuwa imejitoa na mtu ambaye amekuwa akichafua nembo ya klabu hiyo mara kwa mara.

MATUKIO YA UTATA YA SUAREZ
Februari 2007: Suarez alicheza mechi yake ya kwanza kimataifa akiwa na kikosi cha Uruguay katika mchezo dhidi ya Colombia, lakini alitupwa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya mwisho, baada ya kuonyeshwa kadi ya njano ya pili kutokana na mambo ya kijinga.

Novemba 2007: Alijiunga na Ajax akitokea Nacional ya Uruguay, lakini baadaye aliadhibiwa na klabu hiyo ya Uholanzi, baada ya kugombana na mchezaji mwenzake, Albert Luque, kwenye vyumba vya kubadilishia wakati wa mapumziko.

Julai 2010: Wakati wa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Dunia 2010, Suarez alidaka kwa makusudi mpira uliokuwa ukielekea kwenye nyavu uliopigwa na Dominic Adiyiah wa Ghana na hivyo kuonyeshwa kadi nyekundu. Penalti ilitolewa na Asamoah Gyan akakosa na baada ya hapo, Suarez alionekana akishangilia.

Novemba 2010: Suarez alifungiwa mechi saba na Chama cha soka cha Uholanzi na kutozwa faini na klabu yake kutokana na kumng'ata shingoni kiungo wa PSV Eindhoven, Otman Bakkal katika mchezo wa Ligi Kuu ya nchi hiyo Eredivisie.

Oktoba 2011: Baada ya uhamisho wake wa kutua Liverpool, Januari 2011, aligongwa kidogo sana na kiungo, Jack Rodwell, aliyekuwa akichezea Everton kipindi hicho na Suarez akajiangusha kama vile amefanyiwa rafu mbaya. Rodwell alitolewa nje kwa kadi nyekundu.
Oktoba 2011: Suarez aliingia kwenye madai ya kumfanyia ubaguzi beki wa Man United, Patrice Evra katika mchezo wa Ligi Kuu. Suarez baadaye akakutwa na hatia na hivyo kufungiwa mechi nane na faini ya pauni 40,000.

Desemba 2011: Alionekana akiwafanyia kituko mashabiki wa Fulham. Kwa kipindi hicho, tayari alikuwa anachunguzwa na FA kutokana na tukio la ubaguzi, licha ya kwamba alikuwa bado hajaadhibiwa, lakini jambo hilo lilimfanya aongezewe mechi moja zaidi.
Februari 2012: United na Liverpool zilikutana katika Uwanja wa Old Trafford, lakini kuliibuka utata hapo baada ya Suarez kukataa kupeana mkono na Evra kabla ya mechi hiyo kuanza.

Oktoba 2012: Alishangilia bao alilowafunga Everton kwa staili ya kupiga mbizi mbele ya kocha wa Toffees, David Moyes, ambaye mapema alidai kuwa na sheria kali za kuwabana wachezaji wanaojiangusha kama Suarez, ambao wanachafua soka la England.
Januari 2013: Aliunawa mpira kabla ya kufunga bao la ushindi katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA huko Mansfield.

Aprili 2013: Alimng'ata mkononi Branislav Ivanovic, lakini hakuweza kuadhibiwa kwasababu mwamuzi hakuwa ameliona tukio hilo katika mechi, ambapo Liverpool ilifunga bao la kusawazisha katika dakika za majeruhi na hivyo mchezo huo kumalizika kwa sare ya 2-2.

No comments:

Post a Comment