Pages

Thursday, April 25, 2013

JAVI MARTENEZ: NIDHAMU NA MFUMO NDIO VILIIUA BARCELONA

Javi Martínez akimruka Sergio Busquets  kwenye mchezo wao wa juzi

MUNICH, Ujerumani
BAYERN Munich wameishushia Barcelona kipigo cha mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Allianz Arena, juzi usiku kwenye nusu fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mabingwa hao wapya wa Bundesliga, walionyesha kiwango ambacho kinaingia kwenye historia na kuiangushia kipigo cha mbwa mwizi Barca, ambayo inatajwa kama moja ya timu bora zaidi duniani.
Tuchambue kiwango cha Bayern.

Mfumo
Bayern waliingia uwanjani wakitumia mfumo wa kujilinda wa 4-2-3-1, kuna wakati walikosa mshambuliaji wa kweli, Barcelona wao walitumia mfumo wao wa kawaida wa 4-3-3.
Lionel Messi alikuwa fiti kucheza, Mario Gomez alichukua nafasi ya Mario Mandzukic aliyekuwa na adhabu na Arjen Robben alianza kulia. Jerome Boateng na Alexis Sanchez, walianza kinyume na matarajio ya wengi kwenye timu zote mbili.

Mpango wa awali
Barca walianza kwa kumiliki sehemu kubwa ya mchezo, wakipigiana pasi kwenye nusu yao, katika harakati za kupima kasi ya Bayern.
Wajerumani hao waliwaruhusu Gerard Pique na Marc Bartra kumiliki mpira na kujisahau, lakini wachezaji wengine wote wa Barca walikabwa kwa karibu. Thomas Mueller alitarajiwa kukaba mtu na mtu kwenye kiungo, lakini kazi yake ilibadilika na kufunguka na kuwa huru.

Cha kufurahisha alikuwa, Gomez ambaye alimkaba Sergio Busquets, mtu na mtu. Aliposhuka chini sana alimuacha huru, alipovuka mstari tu na kuingia kwenye nusu ya Bayern, Gomez alimuwahi na kucheza ‘man to man’.
Hili lilimfanya Mueller kuongeza nguvu upande wa kulia wa uwanja, wakati Arjen Robben na Franck Ribery walikuwa wakiwalinda mabeki wa pembeni.
Cha muhimu kutambua hapa ni kuwa mfumo wa Bayern haukuwa ule wa ‘Man to man’ sana, waliwazuga Barca ili wajione wanakabwa hivyo. Bayern walicheza karibu na adui zao wakiwa na mpira, lakini ni wachezaji wachache sana waliokabwa kwa karibu. Waliwalazimisha Barca kucheza kwenye eneo lao, wakati wao (Bayern) walikuwa wakilinda pumzi zao kwa kuepuka kukimbizana na Barca.

Arrigo Sacchi amehusika
Hatari kubwa kwa mfumo huu ni kwamba, Bayern walikabia juu sana, hasa kulinganisha na kasi ya Sanchez, Messi na Pedro. Bayern walielekeza akili yao kwenye kuziba njia za Barca kupitisha mipira, wakati kujipanga vizuri kwa Dante kulizuia mashambulizi ya moja kwa moja kabla hata hayajaanza, staili hii ilikua ikitumiwa na kocha wa zamani wa Italia, Arrigo Sacchi.

Javi Martinez
Kukabia juu, na kupunguza kasi ya Busquets, iliwaruhusu Bayern kumfungulia mnyama wao, Javi Martinez. Mhispaniola huyo wakati akiwa Athletic Bilbao alikuwa hana furaha kila akikutana na Barca, lakini safari hii ameondoka na kiroho kwatu.
Alikuwa akipanda mbele, akiwatia presha viungo wa Barca na kuwapandia kwenye enka zao usiku kucha. Martinez alikaba mipira mara sita na kuingilia pasi mara mbili, kuna wakati mwingine alipanda kusaidia mashambulizi, huku akiwa makini sana.
Bastian Schweinsteiger alishuka chini kidogo wakati Martinez alipopanda mbele, wakati jukumu la Mueller, lilimfanya wakati mwingine kushuka chini na kucheza sambamba naye.

Kipindi cha pili
Martinez alipata kadi ya njano sekunde ya 50 ya kipindi cha pili, baada ya hapo alipunguza kasi. Ilikuwa faulo yake ya tano na alistahili kadi ya njano, hivyo mpango wa mechi ulilazimika kubadilika.
Ni katika kipindi hiki cha pili, ambapo faida ya kutokukimbizana na Barca inaonekana. Wachezaji wa Bayern waliendelea kuonekana hawajachoka licha ya kufanikiwa kuwazuia Barca katika kipindi cha kwanza, kitu ambacho timu nyingi hushindwa.
Wakati ambao Barca walifanikiwa kuingia mchezoni na cha muhimu hapa kujua ni kuwa Barcelona walifanikiwa kuanza kucheza vizuri baada ya Martinez kupata kadi ya njano.
Bayern wajikita zaidi kwenye mfumo wa 4-2-3-1 (au 4-4-1-1, hasa ukiangalia jinsi ambavyo Franck Ribery na Robben walivyokuwa wakishuka chini zaidi) na walitumia kiungo mkabaji aliyekuwa akilinda mabeki.
Philipp Lahm alimzidi ujanja, Jordi Alba kila walipokutana uso kwa uso pembeni ya uwanja na Dante alikuwa na kiwango bora ambacho hutakuja kukiona tena kwa beki wa kati.
Mfumo wa mabeki wa Bayern, ulikuwa sawa na ule uliotumiwa na AC Milan, lakini tofauti pekee ilikuwa ubora na uzoefu. Robben alijituma bila kuchoka na alitisha, alianzisha mashambulizi ya kushtukiza, aliingia na mpira ndani, kwa ufupi alikuwa vizuri.
AC Milan walishindwa kutumia nafasi zao. Lakini Bayern walikuwa na uwezo wa kushinda zaidi ya mabao manne.

Hitimisho
Barca hawakucheza vizuri dhidi ya Paris Saint-Germain na Wafaransa hao walithibitisha kwamba beki wa kati bora, stamina, nidhamu kwenye kiungo ndiyo vitu sahihi vya kuiua Barca.
Bayern walijumlisha kujipanga kama Thiago Silva na Blaise Matuidi, walivyofanya, lakini Wajerumani hao walikuwa na kitu kimoja cha ziada ambacho wote AC Milan na PSG walikosa.
Matokeo haya yalikuwa yakuvutia sana, Barca walifunga mabao manne dhidi ya AC Milan, Camp Nou, lakini ni ngumu kwao kufunga idadi hiyo ya mabao dhidi ya Mashine hizi za Kijerumani.

No comments:

Post a Comment