Pages

Monday, April 29, 2013

HAWA NDIO WANAOIUA SIMBA


KOCHA Mkuu wa zamani wa Simba, Milovan Cirkovic na kiungo wa timu hiyo, Haruna Moshi ‘Boban’ wametajwa kuiua Simba, baada ya kutimuliwa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na jijini jana, Kocha Mkuu wa Kagera Sugar, Abdallah ‘King’ Kibadeni, alisema uongozi wa klabu hiyo, ulifanya makosa makubwa ya kuwatimua nyota watatu wa timu hiyo, ambao ni  Boban na mabeki wao, Amir Maftah na Juma Nyosso.

Kibadeni alisema kilichosababisha Simba ishindwe kutetea ubingwa wao, ni kuwatimua wachezaji hao na kocha wao katikati ya msimu kitu ambacho kiliathiri mfumo mzima wa uchezaji.

Alisema katika mzunguko wa kwanza, Simba ilianza vizuri lakini ilipoteana baadaye baada ya uongozi wa klabu hiyo kubadilisha benchi la ufundi, ambalo lilichukuliwa na Kocha, Patrick Liewig akisaidiana na Jamhuri Kihwelu ‘Julio’.

Kibadeni alisema uongozi wa Simba usingefikia uamuzi wa kumtimua Milovan, pamoja na mgawanyiko ambao umetokea kati yao na wanachama wa tawi la Mpira Pesa kuhusu matokeo mabaya ya ligi hiyo.

“Hakuna mtu wa nje aliyeivurunga Simba, bali ni watu waliopo ndani ya klabu hiyo waliyoivuruga timu hiyo, jambo lingine ni pale kumtimua Milovan tayari alishaandaa kikosi chake na wachezaji waliozoea mfumo wake,” alisema Kibadeni.

Alisema Liewig asingeweza kupata mafanikio ya muda mfupi baada ya kukabidhiwa timu hiyo kutokana na mfumo wake wa ufundishaji.
Kibadeni alisema suala la kuachwa kwa wachezaji wakubwa na kupewa nafasi vijana pekee, hali hiyo ilichangia Simba kuwa na matumaini madogo ya kuibuka na ushindi katika mechi zao.

Simba kwa sasa inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo, huku Yanga ikiwa imechukua ubingwa baada ya kufikisha pointi 56 ambazo hazitafikiwa na timu nyingine.

No comments:

Post a Comment