Dunga |
MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya
soka nchini Kenya, timu ya Tusker wamezinduka baada ya juzi Ismail Dunga kuipa
timu hiyo ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Western Stima katika uwanja wa Afraha.
Hata hivyo haikuwa ushindi rahisi
kwa Tusker, kwani muda mwingi walijikuta wakishambuliwa na Stima na kwamba
washambuliaji wa Stima Dennis Onkangi, Fred Shimonyo na Job Omuse wanapaswa
kutwishwa mzigo wa lawama kwa kushindwa kuipa timu yao ushindi kutokana na
kupoteza nafasi nyingi.
Omuse alipata nafasi mbili za wazi,
lakini alipiga mpira nje huku wenzake nao wakiwa wanapoteza nafasi mara kadhaa
katika kipindi cha kwanza, ambacho timu yao ilicheza vizuri sana na kutawala
kwa sehemu kubwa.
Kipindi cha kwanza ndiyo kilikuwa
kigumu zaidi kwa Tusker, kwani ilikuwa katika wakati mgumu, lakini kipindi cha
pili baada ya kufanya mabadiliko kwa kumuingiza Joshua Oyoo hatimaye
walizinduka na Oyoo alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Stima.
Iliwalizimu Tusker kusubiri hadi
dakika ya 73 wakati ambapo Oyoo alipowahandaa mabeki na kutoa pasi kwa Dunga aliyekuwa
ndani ya eneo la hatari na kisha kuukwamisha mpira wavuni. Kwa ushindi huo
Tusker imepanda hadi katika nafasi ya 12 ya msimamo wa ligi hiyo wakati Stima
imebaki katika nafasi ya tisa kwa kuwa na pointi 11.
No comments:
Post a Comment