TIMU ya Simba
inatarajia kurejea jijini Dar es salam Jumatano ijayo kutoka mjini Arusha ambako imeweka
kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Libolo ya
Angola.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika Jumapili ijayo
(Februari 17) kuanzia saa kumi na nusu jioni. Uongozi unafanya utaratibu wa
kuiwezesha timu kufanya mazoezi katika Uwanja wa Taifa walau mara moja kabla ya
mechi hiyo ili kutoa nafasi kwa benchi la ufundi kutoa maelekezo mahususi kwa
wachezaji kuhusiana na mechi hiyo.
Kocha na mchezaji wa zamani wa Simba, Talib Hilal,
anaelekea Arusha leo ili kuongeza nguvu ya benchi la ufundi la Wekundu wa
Msimbazi. Hii si mara ya kwanza kwa Talib kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi
la Simba kwani alifanya hivyo pia miaka kumi iliyopita wakati klabu hiyo
ilipocheza na Zamalek ya Misri na kufanikiwa kuitoa.
Talib Hilal hajaja kuchukua nafasi ya mtu yeyote
kwenye benchi la ufundi. Amekuja kwa mapenzi yake kwa Simba na mara zote klabu
inamkaribisha kwa vile uwezo wake kitaaluma, uzoefu wake na uwezo wake katika
kuhamasisha unakubalika ndani ya klabu.
Simba SC inaomba washabiki na vyombo vya habari
waisaidie klabu kwa kutotangaza taarifa zenye kuashiria migogoro isiyokuwepo. Simba
wanawakilisha heshima na hadhi ya Tanzania katika mashindano
haya.
Uongozi wa klabu unaomba uzalendo kwa taifa
letu walau katika kipindi hiki. Uongozi
unaomba wadau wake wa vyombo vya habari kuandika habari za kujenga umoja,
mshikamano na uzalendo kwa Watanzania wote ili hatimaye Simba ifanye
vizuri.
No comments:
Post a Comment