BAADA ya sare
mbili mfululizo, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), Simba leo wanashuka Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya
wakiwa wageni wa Tanzania Prisons.
Katika mechi
zake mbili zilizopita, Simba iliondoka pointi mbili tu kati ya sita ilizokuwa
ikizipigania. Ilitoka sare na timu za JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na baadaye sare ya 1-1 ugenini dhidi ya Oljoro JKT.
Hiyo itakuwa
mechi ya nne kwa Mfaransa Patrick Liewig tangu aanze kuinoa Simba huku
akifanikiwa kuondoka na ushindi katika mechi moja dhidi ya African Lyon
inayokamata mkia kwenye ligi hiyo. Simba iliilaza Lyon mabao 3-1.
Kwa upande wa
kocha Jumanne Chale anashusha kikosi chake uwanjani leo akiwa na kumbukumbu
nzuri ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon katika mechi
iliyochezwa kwenye uwanja huo huo Februari 9 mwaka huu.
Hekaheka
nyingine itakuwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza wenye uwezo wa kuchukua
watazamaji 25,000 utakapokuwa mwenyeji wa mechi kati ya Toto Africans na African
Lyon. Wakati Lyon ikikamata mkia, Toto Africans yenye pointi 14 inashika nafasi
ya 12 katika ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
Mwamuzi Simon
Mbelwa wa Pwani atakuwa pilato wa mechi kati ya Coastal Union ya Tanga na
Oljoro JKT ya Arusha itakayofanyika Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Mechi hiyo
inatarajiwa kuwa na upinzani mkubwa kutokana na uhodari wa timu zote
mbili.
Nayo JKT Ruvu
ambayo haijafanya vizuri msimu huu kulinganisha na minne iliyopita itacheza Azam
kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. JKT Ruvu chini ya kocha
Charles Kilinda inakamata nafasi ya nne kutoka chini ikiwa na pointi 16 baada ya
kucheza mechi 15.
Iwapo itafanikiwa kushinda mechi hiyo, Azam itaendelea kujiimarisha katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Yanga. Azam ambayo ni moja ya timu zenye safu kali ya ushambuliaji katika ligi hiyo ikiwa imefunga mabao 27 ina pointi 33.
No comments:
Post a Comment