Pages

Saturday, February 23, 2013

FIFA KUCHUNGUZA KWA KINA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA TFF

OFISA Maendeleo wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi amewahakikishia Watanzania kuwa ujumbe wa Shirikisho hilo utakaokuja nchini mwezi ujao, utafanya uchunguzi wa kina kuhusu mchakato wa uchaguzi wa viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA) na kutoa uamuzi kwa maslahi ya mchezo huo.
“Ninafurahi kwamba hali ya utulivu imefikia kiwango hiki na nina uhakika FIFA itafanya uchunguzi wa kina na kufanya uamuzi kwa maslahi ya mpira wa miguu,” amesema Mamelodi alipokuwa akizungumzia uchaguzi mkuu wa TFF ambao ulikuwa ufanyike Februari 24 mwaka huu lakini ukasimamishwa kutokana na matatizo kadhaa baada ya baadhi ya wagombea kuenguliwa.
Mbali na kuhudhuria Mkutano Mkuu wa TFF na uchaguzi, safari ya Mamelodi nchini pia ilihusisha kumtambulisha msaidizi wake, Patrick Onyango ambaye amejiunga na ofisi hiyo ya FIFA kuanzia mwishoni mwa mwaka jana, kufuatilia miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na GOAL Project 4 ambayo ni uwekaji wa nyasi bandia kwenye Uwanja wa Nyamagana na maendeleo ya Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, mikakati ya mwaka 2013 na kozi mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Mikutano wa TFF jana, Mamelodi alisema uamuzi wa Shirikisho hilo kutuma wajumbe katikati ya mwezi ujao unatokana na mawasiliano baina ya Rais wa TFF, Leodegar Tenga na FIFA ambayo ilitaarifiwa hali halisi ilivyo na kama inaweza kusaidia kutatua matatizo yaliyopo.
“FIFA haitakuja kuingilia mchakato wa uchaguzi, itakuja kutatua matatizo,” amesema Mamelodi. “Masuala ya uchaguzi ni ya ndani ya nchi. FIFA haiji kuichagulia Tanzania rais. Wajumbe wanaweza kumchagua mtu yeyote wanayeona kuwa anafaa kuwa rais,” amesema Mamelodi.
“Lakini katiba ya FIFA iko wazi kwamba mwanachama wake ni lazima akubaliane na sheria za Shirikisho kuwa wanachama ni lazima wabanwe na Katiba ya FIFA. Kwa hiyo mara tu unapopata uanachama wa FIFA, ni lazima ujue kuwa utabanwa na katiba ya FIFA na mojawapo ya mambo haya.
“Lakini kuna tofauti na kitendo cha Serikali kusimamisha uchaguzi kwa kuwa hiyo inakuwa ni Serikali kuingilia moja kwa moja masuala ya mpira wa miguu, kitu ambacho katiba ya FIFA inakataza.”
Mamelodi, ambaye alitumia muda mwingi kuelezea umuhimu wa hali ya utulivu iliyotawala kwa muda mrefu nchini, amesema anajua kuwa uongozi wa Rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga umefanya mengi katika kuhakikisha unajenga mazingira mazuri ya maendeleo ya mpira wa miguu, lakini kuna wakati ni lazima uheshimu uamuzi wa mtu.
“Tenga amesema imetosha anaondoka na hatuna budi kuheshimu uamuzi wake. Hiyo ni kauli inayotoka kwa kiongozi wa kweli, kiongozi anayewajibika. Lakini kwa kuangalia misingi ambayo uongozi wake umeijenga, ni wazi kuwa kiongozi mpya ataendeleza taasisi bila ya matatizo.
“Tanzania haikufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, lakini kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo ilifanyika, mingine ambayo ilijaribiwa kwa mara ya kwanza nchini Tanzania na ikafanikiwa. Kuna Azimio la Bagamoyo, Semina ya Mawasiliano ya Jamii (Comm-Unity) ya Wanawake, Futuro III na mingine. Yote hii ilifanyika kwa sababu kulikuwa na utulivu.
“Hivi sasa TFF ina sekretarieti ina Mkurugenzi wa Ufundi; ina programu za maendeleo na kuna utulivu. Cha msingi ni kuendeleza haya. Kama mambo haya yataendelezwa baada ya uchaguzi, ni dhahiri kuwa mpira utazidi kuendelea. Hakuna njia ya mkato katika maendeleo.”
Uchaguzi wa TFF ulihusisha nafasi za rais, makamu wa rais na wajumbe wa Kamati ya Utendaji kutoka Kanda 13 za Shirikisho.
Angetile Osiah
Katibu Mkuu
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment