Thursday, January 10, 2013
TIMU YA TAIFA "TAIFA STARS" YAWASILI SALAMA ETHIOPIA KUKIPIGA KESHO
KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimefika salama Addis Ababa tayari kwa mechi ya kirafiki dhidi ya wenyeji Ethiopia utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa wa Addis Ababa kuanzia saa 11.30 jioni za Tanzania na Ethiopia
Akizungumza kwa njia ya simu toka Adidis Ababa Afisa Habari wa Shirikisho la soka nchini (TFF) Boniface Wambura alisema, Stars imefikia katika hoteli ya Hilton na wachezaji 16 tayari kwa mchezo huo maalum kwa kuipa maandalizi ya mwisho Ethiopia kabla ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazoanza Januari 19 mwaka huu.
Wachezaji wa Yanga, beki Kevin Yondan na kiungo Frank Domayo watajiunga na kikosi cha timu wakitokea Antalya, Uturuki.
Kocha Mkuu wa Stars, Mdenmark Kim Poulsen na Mholanzi Ernie Brandts wa Yanga, wamekubaliana Yondan na Domayo pekee, kati ya wachezaji watano Yanga walioitwa Stars ndio wajiunge na timu hiyo.
Wachezaji waliopo ni pamoja na Juma Kaseja kutoka Simba ambaye pia ndiye nahodha wa Stars na Aishi Manula (Azam FC), huku kwa upande wa Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Amir Maftah (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), na Shomari Kapombe (Simba).
Wengine ni viungo ni Salum Abubakar (Azam), Amri Kiemba (Simba), Khamis Mcha (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba) na Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), wakati washambuliaji ni Mbwana Samata, Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC) na Mrisho Ngasa (Simba).
Stars ambayo pia itautumia mchezo huo kama sehemu ya maandalizi ya mechi ya mchujo dhidi ya Morocco kuwania tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014, mchezo utakaochezwa Machi mwaka huu.
Katika maandalizi yake hayo, mara ya mwisho Stars ilikwaana na Zambia Desembza 22 mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuibanjua bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment