Pages

Friday, January 11, 2013

JEURI YA FEDHA: ABRAMOVICH KUMVUNJIA BENKI PEP GUARDIOLA SASA KUWA KOCHA GHALI ZAIDI DUNIANI AKITUA CHELSEA

London, England

ROMAN ABRAMOVICH ameamua kuvunja ukimya baada ya kufahamika mpango wake wa kuwa tayari kutoa ofa ya pauni milioni 18 kwa mwaka kwa Pep Guardiola endapo atakubali kutua kuinoa Chelsea katika majira ya joto.

Mmiliki wa 'The Blues', Abramovich anataka kumfanya Guardiola kuwa kocha anayelipwa fedha nyingi zaidi duniani.

Bado hajakata tamaa katika mpango wake wa kumnasa kocha huyo wa zamani wa Barcelona, ingawa atapaswa kupigana kiume na Bayern Munich, Manchester United na Manchester City.

Abramovich atampa ofa Guardiola ya pauni miloni 54 kwa kipindi cha miaka mitatu, mshahara ambao ni zaidi mara mbili ya fedha anayolipwa Sir Alex Ferguson, ambaye kwa sasa ndiye kocha anayeongoza kwa mshahara Uingereza, akiwa anapokea pauni milioni 7.6 kwa mwaka.

Abramovich, ambaye kwa sasa yupo likizo huko Caribbean, inafahamika kwamba amekerwa na kipigo cha Chelsea ilichokipata Jumatano cha mabao 2-0 kwenye mechi ya nusu fainali ya kwanza ya michuano ya Kombe la Ligi dhidi ya Swansea tena ikiwa katika uwanja wao wa Stamford Bridge.

Kocha wa muda, Rafa Benitez kibarua chake kipo salama hadi mwishoni mwa msimu na haijalishi kama ataendelea kushinda au Mhispania mwenzake huyo, Guardiola atakubali kuinoa ama atakataa.

Chanzo kimoja kilichopo karibu na Abramovich, kililiambia the Daily Express: “Roman bado anamhitaji Pep. Ni chaguo lake la kwanza na Chelsea itampa ofa kubwa.

“Benitez ataendelea kubaki hadi mwishoni mwa msimu, jukumu lake kubwa ni kumaliza nafasi ya nne na kushinda kombe.”

Mashabiki wa Chelsea Jumatano wiki hii waliendelea tena kumuweka Benitez katika wakati mgumu ambaye kwa muda wa wiki saba sasa tangu arithi mikoba ya Roberto Di Matteo, amekuwa akikumbana na zomea zomea.

Tayari Guardiola, ambaye majira ya joto yaliyopita alikataa ofa ya miaka mitatu aliyopewa na Abramovich ili kuinoa Chelsea  baada ya kuweka wazi kuwa anahitaji kupumzika kwa mwaka mmoja, sasa ametangaza kurudi rasmi katika kazi ya ukocha mwishoni mwa msimu.


@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

MILAN YAMTUKANA BALOTELI

Manchester, England

MANCHESTER CITY inajiandaa kupokea ofa ya pauni milioni 24 kutoka kwa AC Milan ili kumnasa Mario Balotelli, licha ya awali kumfananisha na 'epo' (apple) lililooza.

Wazo hilo la mmiliki wa Milan, Silvio Berlusconi lilionekana kuwa mwisho wa dili la mshambuliaji huyo mtukutu kurudi Italia.

Wakala wa Balo, Mino Railo alisema: “Mario alimsamehe Berlusconi baada ya kusikia kauli hiyo. Lakini Mario alinitaka kuwa kimya kwa sababu anapendwa na rais wa Manchester City.”

Balotelli, 22, ambaye mashabki wengi wanataka auzwe,  juzi alianza kufanya mazoezi na Man City akiwa amebadili rangi ya nywele zake.

Wiki iliyopita 'Balo' alikunjana na kocha wake, Roberto Mancini katika mazoezi, na sasa City ipo tayari kumuuza endapo itapata mbadala wake sahihi.

@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

ANELKA  ATAKA KUSTAFU

Paris:
NICOLAS ANELKA ambaye kwa sasa ana miaka 33, atatangaza kutundika daluga rasmi baada ya kuondoka Klabu ya Shanghai Shenhua, mshambuliaji huyo amewaeleza marafiki zake.

Anelka ambaye anajulikana kwa jina la utani kama Le Sulk, huku akiwa ameshawahi kuzichezea Arsenal, Liverpool, Man City, Bolton na Chelsea, kwa sasa anajifua chini ya kocha wake wa zamani wa 'The Blues', Carlo Ancelotti akiwa na kikosi cha PSG.
Ancelotti alisema: “Ameomba tu kujifua, sisi ni marafiki.”

@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@@

REDKNAPP KUMSALIMIANA NA LEVY

London:
HARRY REDKNAPP hana tatizo na Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy na amesema atasalimiana naye kwa kupeana mikono kesho watakapokutana wakati QPR ikicheza dhidi ya  timu hiyo kwenye mechi ya Ligi Kuu England .

Redknapp ambaye alitua QPR Novemba mwaka jana, ikiwa ni miezi mitano baada ya kutimuliwa na Levy, alisema: “Kama nitamuona Daniel, nitapeana mikono naye, hakuna tatizo. Siku nilipoanza kazi QPR, simu ya kwanza kuipokea ilikuwa kutoka kwa Daniel akinitakia kila heri katika kazi yangu."

No comments:

Post a Comment