Pages

Wednesday, December 19, 2012

YANGA YAMTEMA KOCHA WA MAKIPA, MWENYEWE AWASHUKURU WANAYANGA KWA USHIRIKIANO WALIOMPA



YANGA imemtema Kocha wa makipa, Mfaume Athumani na kumrejesha Mkenya Razak Siwa, baada ya kumaliza mkataba wa kuifundisha timu hiyo.

Siwa aliyewahi kuwa kocha msaidizi wa timu hiyo, anatarajia kusaini mkataba mpya baada ya Yanga kurejea kutoka Uturuki.

Akizungumza leo, Mfaume alisema kuwa hataambana na kikosi cha timu hiyo kutokana na kumaliza mkataba wake na klabu hiyo ambayo alishawahi kuitumikia katika miaka ya nyuma.

Alisema kuwa, mkataba wake na Yanga umefikia ukingoni, hivyo ameamua kupumzika kwa muda katika masuala ya soka.
 “Nashukuru Wanayanga kwa ujumla wao kwa sababu kwa muda wote ambao nimekuwepo hapa kama mchezaji, niliporejea kama kocha wa makipa wamenipa ushirikiano wa hali ya juu,” alisema Mfaume.

“Kwa sababu hiyo sina sababu ya kutofurahi kutokana na mafanikio ambayo niliyapata nikiwa na Yanga, naamini ni mengi licha ya changamoto nyingi nilizokutana nazo kama kocha,” alisisitiza Kocha huyo.

Alisema kuwa jambo ambalo anaweza kujivunia ni kumfanya kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ kuwa namba moja kwenye kikosi cha Yanga lakini zaidi ni kuunda nguvu kazi ya makipa bora Tanzania kwa sasa.

“Nasema hivyo kwa sababu ukiangalia Berko ambaye ameondoka, amekuwa ni moja ya tunda la kujivunia kwa Wanayanga kwa muda mrefu, pia alikuwepo Shaban Kado pamoja na Said Mohamed ambao wote naamini wanaweza kuwa makipa wa timu za taifa,” alisema Mfaume.

Hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara kumalizika, Yanga imefungwa mabao 12 katika mechi 13 ilizocheza na kujikuta ikipata pointi 29,  jambo lilionyesha kuwa Mfaume alifanya kazi kubwa katika kuwanoa makipa hao.

No comments:

Post a Comment